Kremlin: Jeshi la majini la Russia kuzima 'uharamia' wa Magharibi
Afisa mwandamizi wa Ikulu ya Russia (Kremlin) ameonya kwamba, yumkini jeshi la wanamaji la nchi hiyo likatumwa kuzuia mataifa ya Magharibi kukamata meli za Urusi kama sehemu ya vikwazo dhidi ya usafirishaji wa mafuta ya Moscow.
Nikolai Patrushev, afisa mkuu wa Kremlin anayesimamia usafirishaji wa meli na mpambe wa karibu wa Rais wa Russia, Vladimir Putin, amekuliwa akisema kwamba, kwa hatua yake hiyo ya kuzima 'uharamia' wa Magharibi, Moscow inataka kutuma ujumbe mzito haswa kwa Uingereza, Ufaransa na mataifa ya Baltic.
"Ikiwa hatutapambana kwa uthabiti, Waingereza, Wafaransa, na hata Wabaltiki karibuni watakuwa na ujasiri mkubwa kiasi cha kujaribu kuzuia nchi yetu kufikia bahari, hasa katika Bonde la Atlantiki," ameonya.
Patrushev amesema Russia inabidi iweze kusafirisha mafuta, nafaka na mbolea ili kwa maslahi ya uchumi wake. Amewashutumu maadui wa Russia katika nchi za Magharibi kwa kulenga moja ya sekta muhimu zaidi za uchumi wa Russia, ambao ni usafirishaji wa meli.
Mwezi uliopita wa Januari, Moscow ililaani vikali kitendo cha Marekani cha kukamata meli ya mafuta yenye bendera ya Russia katika Bahari ya Atlantic, na kuitaja hatua hiyo kama ukiukaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Sheria ya Bahari. Jeshi la Marekani lilidai kuwa, meli hiyo ya mafuta ya Marinera ya Russia ilikamatwa "kwa ukiukaji wa vikwazo vya Washington" dhidi ya Venezuela.
Aidha mnamo Septemba 2025, mamlaka za Ufaransa zilitwaa meli nyingine iliyokuwa na mfungamano na Russia kwa jina Boracay, inayodai kuwa na bendera ya Benin. Rais Vladimir Putin alilaani vikali hatua hiyo na kuutaja kuwa "uharamia".