Shambulio la bomu laua watu 50 na kujeruhi 100 harusini Uturuki
Watu wasiopungua 50 wameuawa na wengine wapatao 100 wamejeruhiwa katika shambulio la kigaidi la kujitolea mhanga lililolenga sherehe ya harusi katika mkoa wa Gaziantep ulioko kusini mashariki mwa Uturuki.
Gavana wa Gaziantep Ali Yerlikaya, amesema shambulio hilo la kigaidi lilitokea yapata majira ya saa tano usiku wa kuamkia leo katika eneo la Akdere wilayani Sahin Bey.
Mashuhuda wamesema, wanawake na watoto ni miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo. Imeelezwa kuwa shambulio hilo lilitokea wakati sherehe hiyo ya harusi ilipokuwa inakaribia kumalizika.
Maziko ya baadhi ya waliouawa yalifanyika leo lakini duru za usalama zimeripoti kuwa maiti nyengine zimeshindikana kuzikwa kutokana na kuharibika sana na kushindwa kutambulika mpaka zifanyiwe vipimo vya vinasaba (DNA).
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema kuna uwezekano kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh ndilo lililohusika na shambulio hilo.
Siku ya Alkihamisi iliyopita pia watu wasiopungu sita akiwemo mtoto mdogo waliuawa na wengine zaidi ya 200 walijeruhiwa wakati magari mawili yaliyotegwa mabomu yaliporipuka karibu na kituo cha Polisi cha mji wa Elazig mashariki mwa Uturuki.
Tangu mwaka uliopita, Uturuki imekuwa ikishuhudia mlolongo wa mashambulio ya kigaidi likiwemo la mwezi Juni mwaka huu katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ataturk mjini Istanbul ambapo zaidi ya watu 40 waliuawa. Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh lilitangaza kuhusika na shambulio hilo.../