Erdogan: EU iwe imeijumuisha Uturuki kufikia mwisho wa mwezi huu
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameupa Umoja wa Ulaya hadi mwisho wa mwezi huu uwe umekamilisha mchakato wa nchi hiyo kujiunga na EU.
Erdogan amesema wakati umefika kwa umoja huo kutoa uamuzi wa iwapo Uturuki itajiunga na EU au la na kwamba taifa hilo limechoka na mzaha na karata ya umoja huo. Amesema siasa hizo za uhasama na undumakuwili za viongozi wa nchi za Ulaya zinaendelea hadi sasa dhidi ya Uturuki.
Baada ya jaribio la mapinduzi ya kijeshi lililofeli, Rais Erdogan alisema Magharibi inaunga mkono ugaidi na kwamba senario ya jaribio hilo la mapinduzi nchini kwake iliratibiwa nje ya nchi.
Alisisitiza kuwa viongozi wa EU wamekuwa wakitoa matamshi yasiyoeleweka juu ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli yaliyotekelezwa na askari wa nchi hiyo Julai 15.
Aidha İsmail Kahraman, Spika wa Bunge la Uturuki hivi karibuni alisema kuwa, katika kipindi cha mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli, nchi za EU ziliitenga nchi yake badala ya umoja huo kuwa pamoja na raia wa nchi hiyo ambao walifanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuhifadhi demokrasia nchini mwao.