Erdogan: Tutawanyonga waliohusika na jaribio la mapinduzi
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema serikali yake inapania kurejesha adhabu ya kifo kwa ajili ya kuwahukumu waliohusika na jaribio la mapinduzi lililofeli mwezi Julai mwaka huu.
Erdogan amesema serikali yake itawasilisha muswada katika bunge la nchi hiyo ili kufufua hukumu hiyo, ambayo ilipigwa marufuku miaka miwili iliyopita, ikiwa ni katika juhudi za Uturuki za kutaka kujumuishwa kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya EU. Amesema: "Tutawasilisha pendekezo hilo bungeni na nina uhakika kuwa litapasishwa na kisha kurejeshwa kwangu ili niliidhinishe kuwa sheria."
Hii ni katika hali ambayo, mashirika ya kutetea haki za binadamu na asasi za kiraia zimeitaka serikali ya Ankara kujiepusha kufanya aina yoyote ya ukatili au umwagaji damu kutokana na ulipizaji kisasi dhidi ya askari na shakshia wanaodaiwa kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi.
Rais Erdogan amekuwa akisisitiza kuwa, jaribio hilo la mapinduzi lilifanywa na nchi za Magharibi na kwamba tukio hilo lisingeweza kuongozwa na kuratibiwa kutoka ndani ya nchi tu. Uturuki kwa mara nyingine tena imeitaka Marekani imkabidhi Fethullah Gülen, kiongozi wa kidini na mpinzani wa serikali ya Rais Recep Tayyip Erdoğan, ambaye anaishi uhamishoni katika jimbo la Pennsylvania, nchini Marekani ikisisitiza kuwa ndiye aliyepanga na kuratibu mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli ya tarehe 15 Julai nchini Uturuki.
Watu wasiopungua 246 waliuawa huku wengine zaidi ya 2,100 wakijeruhiwa katika jaribio hilo la mapinduzi ya kijeshi la Julai mwaka huu. Aidha maelfu ya wafanyakazi wa serikali wakiwemo walimu wamesimamishwa kazi kufuatia tukio hilo.