UNICEF: Hujuma dhidi ya watoto Myanmar inatia wasi wasi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i19204-unicef_hujuma_dhidi_ya_watoto_myanmar_inatia_wasi_wasi
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umeeleza wasi wasi wake kuhusu jinai za kutisha dhidi ya watoto zinazotekelezwa na jeshi la Myanmar katika jimbo la Rakhine.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 10, 2016 13:28 UTC
  • UNICEF: Hujuma dhidi ya watoto Myanmar inatia wasi wasi

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umeeleza wasi wasi wake kuhusu jinai za kutisha dhidi ya watoto zinazotekelezwa na jeshi la Myanmar katika jimbo la Rakhine.

Taarifa ya UNICEF imesema kuwa, mwenendo wa wanajeshi wa kuwashambulia watoto wadogo wa Rohingya kaskazini mwa jimbo la Rakhine ni wa kutisha na kwamba taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa imepokea ripoti za kunajisiwa na kudhalilishwa watoto wadogo katika eneo hilo.

Tangu Oktoba 9, eneo hilo limekuwa chini ya mzingiro wa maafisa usalama wa Myanmar, baada ya kuuawa maafisa tisa wa polisi; mauaji ambayo serikali inadai yalitekelezwa na Waislamu wa kabila la Rohingya.

Wanawake na watoto wa Rohingya wakitoroka jinai za vyombo vya usalama

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema maafisa usalama katika eneo hilo mbali na kutekeleza mauaji dhidi ya Waislamu walio wachache, lakini pia wanawabaka wanawake na mabinti wadogo sambamba na kuwasweka mbaroni Waislamu wasio na hatia.

Katika miaka ya hivi karibuni, Waislamu wengi wa kabila la Rohingya nchini Myamnar wameuawa au kulazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi za Thailand, Malaysia na Indonesia kutokana na hujuma za kutisha za Mabudha wenye misimamo ya kufurutu mpaka wanaoungwa mkono na serikali ya nchi hiyo.