Erdogan: EU inafanya njama ya kutoijumuisha Uturuki katika umoja huo
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema Umoja wa Ulaya unafanya njama ya kuishinikiza nchi yake iachane na mchakato wa kujiunga na umoja huo.
Katika mahojiano na gazeti la Hurriyet la nchi hiyo, Rais Erdogan amesema EU inataka kuilazimisha Uturuki iachane na mchakato wa kujiunga na umoja huo huku akiutaka umoja huo utangaze msimamo wake kuhusiana na kadhia hiyo. Amesema subira ya Waturuki inaelekea ukingoni na wakati umefika kwa EU kuamua iwapo ina nia ya kweli ya kutaka Uturuki ijiunge nayo au la.
Kadhalika kwa mara nyingine tena Rais wa Uturuki ametishia kuwa yumkini nchi hiyo karibuni hivi itaitisha kura maoni kuamua iwapo iendelee na mchakato wa kujiunga na Umoja wa Ulaya au la.
Mapema mwezi Oktoba mwaka huu Rais wa Uturuki aliupa Umoja wa Ulaya hadi mwisho wa mwezi huo uwe umekamilisha mchakato wa nchi hiyo kujiunga na EU na kubainisha kuwa, taifa hilo limechoka na mzaha wa umoja huo.
Amesema siasa hizo za uhasama na undumakuwili za viongozi wa nchi za Ulaya zinaendelea hadi sasa dhidi ya Uturuki. Rais Erdogan ambaye alidai kuwa mapinduzi yaliyofeli ya kijeshi nchini humo yalipangwa na nchi za Magharibi amesisitiza kuwa viongozi wa EU wamekuwa wakitoa matamshi yasiyoeleweka juu ya mapinduzi hayo ya Julai 15.