Mkulima wa ndizi ashinda uchaguzi wa rais nchini Haiti
https://parstoday.ir/sw/news/world-i20413-mkulima_wa_ndizi_ashinda_uchaguzi_wa_rais_nchini_haiti
Jovenel Moise, mkulima wa ndizi na mfanyabiashara mashuhuri ameibuka mshindi katika uchaguzi wa rais nchini Haiti.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 29, 2016 09:46 UTC
  • Mkulima wa ndizi ashinda uchaguzi wa rais nchini Haiti

Jovenel Moise, mkulima wa ndizi na mfanyabiashara mashuhuri ameibuka mshindi katika uchaguzi wa rais nchini Haiti.

Moise mwenye umri wa miaka 48 wa chama cha PHTK ameshinda duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais kwa kupata asilimia 55.67 ya kura sahihi zilizopigwa katika uchaguzi wa Novemba 20 na hivyo uchaguzi huo kuepuka kuingia duru ya pili.

Mfanyabiashara huyo mwenye shirika la kuuza ndizi nje ya nchi amembwaga mpinzani wake wa karibu Jude Celestin wa chama cha LAPEH aliyepata asilimia 19.52 ya kura.

Mwananchi wa kisiwa cha Haiti akipiga kura

Hata hivyo matokeo rasmi ya uchaguzi huo yanatazamiwa kutolewa rasmi Disemba 29, ambapo wagombea wa kiti cha rais na bunge kwa sasa wana fursa ya kwenda mahakamani kupinga matokeo hayo iwapo wana ushahidi kwamba uligubikwana kasoro na uchakachuaji.

Uchaguzi huu ulipasa kufanyika mwezi uliopita wa Oktoba, lakini ukaakhirishwa kutokana na kimbunga cha Matthew kilichoua mamia ya watu mbali na kubomoa majumba na miundomsingi na kusababisha hasara kubwa.

Sehemu ya athari za kimbunga Matthew huko Haiti, mwezi Oktoba

Awali uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Oktoba mwaka jana, lakini ukakosa kufanyika kutokana na migogoro na mivutano ya kisiasa katika kisiwa hicho. Kufuatia hali hiyo Mkuu wa Bunge la Seneti Jocelerme Privert aliteuliwa kuwa kaimu rais, kuchukua nafasi ya Michel Martelly, ambaye muda wake wa kuhudumu ulimalizika Februari 2015.