Nchi za jumuiya ya Francophone zasisitiza udharura wa kupambana na ugaidi
Washiriki katika mkutano wa kimataifa wa 16 wa Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Kifaransa (Francophone) wametilia mkazo udharura wa kupambana na ugaidi na kuanzisha ulimwengu wenye amani na usalama.
Mkutano wa kimataifa wa 16 wa Jumuiya ya Nchi Zinazozungumza Kifaransa umemalizika nchini Madagascar baada ya mashauriano ya siku mbili juu ya ukosefu wa amani na vitisho vya ugaidi kote duniani hususan katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Washiriki katika mkutano huo wametangaza uungaji mkono wao kwa azimio lililopasishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Julai mwaka huu wa 2016 linalosisitiza umuhimu wa kuwepo stratijia na mkakati wa kukabiliana na ugaidi na makundi yenye misimamo yenye kufurutu mipaka. Karibu marais na mawaziri wakuu 20 na maafisa wa ngazi za juu wa nchi wanachama katika jumuiya Francophone wameshiriki katika mkutano wa Madagascar ambao umepasisha maazimio 13 katika nyanja mbalimbali hususan masuala ya ustawi na maendeleo ya kiuchumi.
Japokuwa sababu kuu ya kuundwa jumuiya ya Francophone ni ushirikiano wa nchi wanachama katika masuala ya lugha, lakini katika miaka ya hivi karibuni nchi wanachama zilipanua zaidi uwanja wa ushirikiano wao na kugusa masuala ya kisiasa na kijamii. Wanachama wa jumuiya hiyo wanasema, usalama na amani na kuboreshwa hali ya uchumi katika nchi hizo kunaweza kuwa na taathira kubwa katika masuala mengine ikiwemo lugha. Kwa msingi huo mkutano wa Madagascar ulijadili changamoto za kiuchumi, utayarishaji wa ramani ya njia ya uchumi kabambe na uchunguzi wa njia za utatuzi wa matatizo ya kisiasa na kijamii katika nchi wanachama.
Ufaransa, Niger na Mali ni miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya ya Francophone ambazo tangu mwaka uliopita wa 2015 zimekumbwa na mashambulizi kadhaa ya kigaidi. Mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram katika nchi ya Niger yameua makumi ya watu wasio na hatia na yangali yanaendelea. Nchini Mali makundi ya kigaidi pia yanaendelea kufanya mashambulizi katika miji na maeneo mbalimbali na kuua watu, suala ambalo limevuruga usalama na amani ya nchi hiyo na nchi jirani.
Kwa muda sasa ugaidi umeziathiri nchi nyingi za Afrika lakini mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea barani Ulaya hususan Ufaransa na kuua makumi ya raia wa nchi hiyo yamezidisha udharura wa kujadiliwa kadhia ya ugaidi na jinsi ya kupambana na uovu huo katika upeo wa dunia nzima. Kwa msingi huo katika hotuba yake kwenye mkutano wa Antananarivo, Rais François Hollande wa Ufaransa ametoa wito wa kuanzishwa mtandao wa kupambana na makundi yenye kufurutu mipaka na kusema: Mtandao huo unaweza kuchukua hatua katika nyanja za kubadilishana habari za kipelelezi, kupeana mbinu za kukabiliana na magaidi na kutekeleza operesheni mbalimbali popote pale dhidi ya magaidi iwapo italazimu kufanya hivyo.
Mbali na ugaidi, suala ya ushirikiano wa kiuchumi na njia za kuboresha uchumi limejadiliwa katika mkutano wa Antananario. Ingawa ripoti zinazohusiana na uchumi za miaka iliyopita zimeonesha kuwa, kumekuwepo ustawi mzuri wa kiuchumi katika nchi wanachama wa jumuiya ya Francophone, lakini kutokana na sababu mbalimbali kiwa ni pamoja na kushuka kwa bei ya mafuta ya petroli, kushadidi vita na mapigano ya ndani na mabadiliko ya hali ya hewa na taathira zake mbaya kwa uchumi na uwekezaji, nchi hizo sasa zinakabiliwa na mfumuko wa bei, ukosefu wa ajira na umaskini. Kwa swababu hiyo miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa katika mkutano wa Madagascar ni njia za ustawi endelevu na ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi wanachama.
Mkutano wa Antananarivo ulikuwa fusra ya kujadili na kubadilishana mawazo kuhusu masuala ya uchumi na kupambana na ugaidi. Hata hivyo inaonekana kuwa, mafanikio katika masuala hayo yanahitaji hatua kubwa zaidi ya maamuzi na maazimio yaliyochukuliwa katika mkutano huo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kwa mfano tu, mapambano dhidi ya ugaidi yatafanikiwa pale nchi zote duniani zitakapoazimia kweli kupambana na uovu huo bila ya kujali, lugha, dini, mbari na maslahi yao ya kisiasa na kiuchumi na kuweka kando siasa zao za kikoloni na za kupenda kujitanua.