CIA yamuonya Trump dhidi ya kukiuka makubaliano ya nyuklia ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i20491-cia_yamuonya_trump_dhidi_ya_kukiuka_makubaliano_ya_nyuklia_ya_iran
Shirika la Kijasusi la Marekani CIA limemuonya rais-mteule wa nchi hiyo Donald Trump dhidi ya kukiuka makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 30, 2016 11:08 UTC
  • CIA yamuonya Trump dhidi ya kukiuka makubaliano ya nyuklia ya Iran

Shirika la Kijasusi la Marekani CIA limemuonya rais-mteule wa nchi hiyo Donald Trump dhidi ya kukiuka makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1.

Katika mahojiano aliyofanyiwa na shirika la habari la BBC, John Brennan, Mkuu wa CIA amesema, iwapo Trump atayafuta makubaliano hayo kama alivyoahidi, hicho kitakuwa ni 'kilele cha upumbavu' na ni hatua itakayokuwa na madhara makubwa.

Brennan ambaye atamaliza muda wake wa kuiongoza CIA mwezi Januari mwakani, baada ya kuliongoza shirika hilo la kijasusi kwa miaka minne ameongeza kuwa, ni jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya Marekani, kwa utawala mmoja kufuta na kubatilisha makubaliano yaliyofikiwa na tawala zilizoutangulia.

Rais mteule wa Marekani, Donald Trump

Trump aliwahi kusema wakati wa kampeni za uchaguzi wa rais kuwa, mapatano ya nyuklia ya Iran ni 'maafa  na ni mapatano mabaya zaidi duniani' na kuahidi kuyachana katika siku yake ya kwanza atakapoingia kwenye Ikulu ya White House.

Hata hivyo katika hatua inayoonekana ni ya kulegeza msimamo, Walid Phares, mshauri wa Trump katika masuala ya sera za kigeni akizungumza baada ya ushindi wa mwanasiasa huyo wa chama cha Republican, alisema kunapaswa kufanyika mazungumzo kwanza ya kutathmini upya mapatano hayo.

Makubaliano ya nyuklia ya Vienna

Hii ni katika hali ambayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa, ina machaguo kadhaa ya kufanya iwapo makubaliano hayo hayataheshimiwa.

Haya yanajiri wiki mbili baada ya Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya kusema, makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 hayawezi kubatilishwa na serikali moja kwa kuwa yana baraka kamili ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.