Iran, UN zalaani mauaji ya balozi wa Russia nchini Uturuki
https://parstoday.ir/sw/news/world-i21775-iran_un_zalaani_mauaji_ya_balozi_wa_russia_nchini_uturuki
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali mauaji ya balozi wa Russia nchini Uturuki na kuutaja ukatili huo kama kitendo cha kikatili na kishenzi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 20, 2016 04:23 UTC
  • Iran, UN zalaani mauaji ya balozi wa Russia nchini Uturuki

Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali mauaji ya balozi wa Russia nchini Uturuki na kuutaja ukatili huo kama kitendo cha kikatili na kishenzi.

Bahram Qassemi, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kitendo hicho kinadhihirisha namna magaidi wa makundi ya kitakfiri na yenye misimamo ya kufurutu ada hawana mpaka, viwango, kanuni wala ufahamu wowote kuhusu sheria za kimataifa na masuala ya kidiplomasia.

Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kusimama na kushirikiana na mataifa na serikali katika eneo na kimataifa, ili kuhakikisha kuwa saratani ya ugaidi inasambaratishwa kikamilifu.

Stephane Dujarric, msemaji wa Umoja wa Mataifa

Wakati huo huo, Stephane Dujarric, msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema umoja huo unalaani mauaji hayo ya kikatili na kubainisha kuwa, hakuna jambo lolote linaloweza kuhahalisha mauaji dhidi ya mabalozi na wanadiplomasia na kusisitiza kuwa sharti wahusika wa jinai hiyo wawajibishwe.

Hapo jana Andrey Karlov, balozi wa Russia nchini Uturuki aliuawa kwa kumiminiwa risasi na mtu aliyetajwa kuwa afisa wa polisi ya Uturuki, alipokuwa akihutubu katika maonyesho ya sanaa ya picha katika mji mkuu wa nchi hiyo Ankara.

Mauaji ya kutisha ya balozi wa Russia nchini Uturuki

Huku hayo yakiripotiwa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki amesema kuwa, mkutano wa pande tatu kati ya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Iran na Russia utafanyika hii leo kama ulivyopangwa, licha ya mauaji ya mwanadiplomasia huyo, ambaye amekuwa mjini Ankara tangu mwaka 2013.