Iran yaandikia UN Barua kuwatetea Waislamu wa Rohingya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i22984-iran_yaandikia_un_barua_kuwatetea_waislamu_wa_rohingya
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif amemuandikia barua katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akitaka umoja huo uzingatie zaidi hali mbaya ya Waislamu wa kabila la Rohingya wanaoteswa na kuangamizwa nchini Myanmar.
(last modified 2026-03-27T07:58:19+00:00 )
Jan 07, 2017 01:09 UTC
  • Zarif
    Zarif

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Mohammad Javad Zarif amemuandikia barua katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akitaka umoja huo uzingatie zaidi hali mbaya ya Waislamu wa kabila la Rohingya wanaoteswa na kuangamizwa nchini Myanmar.

Katika barua yake hiyo, Zarif amebainisha wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya Waislamu wa kabila la Rohingya na kuongeza kuwa: "Serikali ya Myanmar inapaswa kufahamishwa udharura wa kusitisha mara moja ukiukwaji wa haki za Waislamu sambamba na kuhakikisha wanapata misaada ya haraka ya kibinadamu."

Katika barua hiyo kwa Guterres, Zarif ameongeza kuwa: "Waislamu Warohingya mbali na kuwa wamepokonywa haki yao ya kimsingi ya kuwa wenyeji wa ardhi yao, kila siku wanakabiliwa na mauaji na mateso huku idadi kubwa miongoni mwao wakiwa wakimbizi katika nchi zingine."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika barua yake ameongeza kuwa, hali ya Waislamu Warohingya ni kinyume kabisa na hati ya Umoja wa Mataifa na mikataba ya kimsingi ya haki za binadamu. Amesema hali ya kusikitisha ya Waislamu hao ni jambo ambalo limewatia wasi wasi mkubwa Waislamu duniani. Waziri Zarif amesema kuvunjiwa haki za kimsingi Waislamu Warohingya ni jambo linaloweza kuvuruga uthabiti na usalama nchini humo na pia katika nchi jirani.

Waislamu wa Myanmar wakikimbia nchi yao kutokana na mateso wanayoyapata

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameseama anataraji jamii ya kimatiafa na serikali ya Myanmar itachukua hatua ili kuzuia Mabudha wenye misimamo mikali kuwakandamiza Waislamu.

Tangu mwaka 2012 Mabudha wenye misimamo mikali wakisaidiwa na maafisa usalama wa Myanmar wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali za ukatili, mauaji na kubaka wanawake Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini humo. Aidha Mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada wamekuwa wakiwaangamiza kwa umati Waislamu nchini humo. Serikali ya Myanmar imekataa kuwapa uraia Waislamu wa jamii ya Rohingya wapatao milioni 1.1 na kuwataja kuwa wahamiaji haramu kutoka Bangladesh.