Waislamu wa Myanmar wanatarajia mabadiliko chanya nchini
https://parstoday.ir/sw/news/world-i23809-waislamu_wa_myanmar_wanatarajia_mabadiliko_chanya_nchini
Ziara ya siku tatu iliyofanywa huko Myanmar na Yanghee Lee Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuchunguza hali ya Waislamu katika jimbo la Rakhine nchini humo imewapa matumaini Waislamu kuwa huenda hali yao ikaboreka.
(last modified 2026-02-15T09:07:51+00:00 )
Jan 18, 2017 08:11 UTC

Ziara ya siku tatu iliyofanywa huko Myanmar na Yanghee Lee Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuchunguza hali ya Waislamu katika jimbo la Rakhine nchini humo imewapa matumaini Waislamu kuwa huenda hali yao ikaboreka.

Kuanzia mwaka 2009 hadi sasa Mynamar imekumbwa na silsila ya matukio muhimu ya kisiasa na kijamii; na ilitazamiwa kuwa Waislamu pia wangefaidika na mabadliko hayo, hata hivyo kinyume na mtazamo huo wamekuwa wakikabiliwa na ubaguzi, mateso, kuwa wakimbizi na kubaki bila ya makazi. Zaidi ya hayo, Waislamu wa Rohingya huko Myanmar wamekuwa wahanga wa vitendo vya utumiaji mabavu vinavyofanywa na makundi yenye misimamo mikali nchini humo. Waislamu hao hata kama wamekuwa wakifuata njia ya kuwa na subira na uvimilivu, lakini pia wanatambua vyema michezo ya kisiasa ya nyuma ya pazia na ni kwa nini San Suu Kyi, kiongozi wa ngazi ya juu wa nchi hiyo, angali anatilia mkazo mchakato wa ubaguzi na kutokuwa tayari kutambua rasmi haki za kiraia za jamii hiyo ya Waislamu wa Rohingya licha ya kudai kutetea demokrasia nchini humo. 

 

Aung San Su Kyi 

Waislamu wa Myanmar wanafahamu pia kwamba upuuzaji wa Umoja wa Mataifa katika kufuatilia hali zao unahusiana na siasa za Marekani na muundo dhaifu na wenye dosari wa taasisi hiyo ya kimataifa. Hata hivyo baada ya kuongezeka mashinikizo ya fikra za waliowengi kieneo na kimataifa, jamii ya kimataifa imeshuhudia kuongezeka kwa kiwango fulani harakati za kidiplomasia za taasisi za kutetea haki za binadamu khususan Umoja wa Mataifa na pia Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Kiislamu (OIC) kwa ajili ya kuchunguza hali inayowakabili Waislamu huko Myanmar. Hii ni katika hali ambayo wimbi la mshikamano ulioonyeshwa na Mamilioni ya Waislamu katika eneo na duniani kote kwa wenzao wa Myanmar limezidisha udharura wa kufuatiliwa hali ya Waislamu wa nchi hiyo. Katika mazingira hayo, Yanghee Lee Mjumbe wa Umoja wa Mataifa amefanya ziara huko Myanmar ili kuchunguza hali ya Waislamu hao.

Waislamu wa Rohingya wakipinga kuuliwa na Mabudha 

 Hata hivyo Ripota Maalumu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa katika safari yake  hiyo ya siku tatu huko Myanmar amezuiwa kuyazuru baadhi ya maeneo katika jimbo la Rakhine. Ikihalalisha hatua yake hiyo, serikali ya Myanmar imesema kuwa ilifanya hivyo kutokana na wasiwasi wa kiusalama. Katika ripoti nyingine imeelezwa kuwa Bi Lee aliruhusiwa tu kufanya mazungumzo na watu waliochaguliwa na serikali ya Myanmar wakati alipozitembelea wilaya za jimbo la Rakhine. Hakuna shaka kuwa vizuizi na mibano hiyo itaathiri pakubwa uchunguzi wa mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa. Hasa ikitiliwa maanani kwamba kushindwa kupata  Bi Lee  kile ambacho kilihitajika kwa ajili ya kufanikisha uchunguzi wake kutatatiza kazi yake hiyo. Pamoja na hayo tunaweza kusema kuwa huenda kuwasili Mjumbe wa Umoja wa Mataiufa huko Myanmar ikawa ni nukta ya kupatikana mabadiliko chanya kwa maslahi ya Waislamu. Hata hivyo matarajio hayo yanaweza kusalia kuwa matupu tu iwapo Umoja wa Mataifa utashindwa kutekeleza majukumu yake ya usimamizi na uongozi, kama unavyotakiwa kufanya kisheria.