Mauaji ya Waislamu msikitini Canada yaendelea kulaaniwa
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu amesema makundi fisadi na ya kibepari yaliyo nyuma ya pazia yanapaswa kuwajibishwa kufuatia mauaji ya Waislamu dani ya msikiti huko Quebec Canada na maeneo mengine ya dunia.
Ayatullah Muhsin Araki, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu ametoa tamko na sambamba na kulaani mauaji ya Waislamu sita katika msikiti mmoja huko Quebec Canada, amesema, Waislamu na mataifa huru kote duniani wameumizwa na jinai ya kigaidi iliyofanywa dhidi ya Waislamu waliokuwa wakisali msikitini nchini Canada.
Ayatullah Araki ameongeza kuwa, makundi ya kigaidi yenye misimamo mikali hayana uhusiano wowote na dini za mbinguni na kwamba leo dunia inahitaji kupambana na ugaidi kiuhakika.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu yenye makao yake hapa mjini Tehran amesisitiza kuwa, haiwezekani kupambana na ugaidi kwa misimamo ya kindumakuwili.
Amesema nchi za Magharibi na hasa Marekani ndio waungaji mkono wakuu wa makundi ya kigaidi duniani ambayo yameanzishwa kwa ajili ya kutimiza malengo ya madola hayo. Amesema madola hayo ya Magharibi yanapaswa kufahamu kuwa kuunga mkono ugaidi ni jambo linalohatarisha usalama wa maeneo yote duniani.
Ikumbukwe kuwa, Jumapili tarehe 29 Januari, gaidi mmoja Mkristo mwenye misimamo mikali na ambaye pia ni muungaji mkono wa Rais Donald Trump wa Marekani, aliingia msikitini wakati wa sala ya Isha huko Quebec Canada na kuwafyatualia risasi Waislamu na kuwaua sita miongoni mwao na kuwajeruhi wengine wengi.