Feb 12, 2017 07:18 UTC
  • Misikiti 91 imeshambuliwa na watu wenye chuki dhidi ya Uislamu Ujerumani

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani imesema misikiti 91 na vituo vya dini ya Kiislamu vilishambuliwa nchini humo mwaka jana pekee 2016.

Shirika la la habari la Associated Press limeripoti kuwa, kwa mujibu wa data za polisi nchini Ujerumani, aghalabu ya visa vya kuhujumiwa misikiti na vituo vya kidini vimefanyika katika jimbo la North Rhine-Westphalia, magharibi mwa nchi. Ripoti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani imebainisha kuwa, kati ya visa 91 vya kushambuliwa misikiti nchini humo, 21 vimefanyika katika eneo hilo la North Rhine-Westphalia ambalo ni mwenyeji wa idadi kubwa ya wahamiaji Waislamu nchini humo. 

Mapema mwezi huu, kituo cha Kiislamu cha mji wa Bielefeld nchini Ujerumani kilichomwa moto ikiwa ni mwendelezo wa wimbi la chuki za kidini dhidi ya Waislamu nchini humo. Mashambulizi dhidi ya Waislamu na maeneo yao ya ibada yameongezeka sana barani Ulaya katika miaka ya hivi karibuni.

Chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu Ufaransa

Mashambulizi dhidi ya Waislamu na maeneo yao ya ibada na ya shughuli zao mbalimbali, yameongezeka sana katika siku za hivi karibuni huko Ujerumani.

Genge lenye chuki za kidini lijulikanalo kwa jina la PEGIDA limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Waislamu nchini Ujerumani.

Ripoti hiyo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ujerumani imeongeza kuwa mwaka 2014, visa 24 vya kushambuliwa misikiti huko Ujerumani viliripotiwa huku mwaka 2015 ukishuhudia visa 75 vya mashambulizi dhidi ya misikiti na vituo vya Kiislamu huko Ujerumani.

Tags