Ukandamizaji wa jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu wa Rohingya
Yanghee Lee, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa ambaye hivi karibuni alizitembelea kambi za Waislamu wa Rohingya huko nchini Bangladesh ametoa taarifa inayoeleza kuwa, jeshi la Myanmar limefanya ukandamizaji na vitendo vya kinyama dhidi ya Waislamu hao.
Mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, kiwango cha ukandamizaji na unyama huo ni kikubwa zaidi kuliko ilivyokuwa ikidhaniwa hadi sasa. Aidha Yanghee Lee, amesisitiza kuwa, wanajeshi wa Myanmar wamewabaka kwa umati wanawake wa Kiislamu wa jamii ya Rohingya na baadhi ya wanaume na wanawake Waislamu wa jamii hiyo wamechinjwa huku watoto wao wakitupwa kwenye moto mkali wakiwa hai.
Matamshi hayo ya kutikisa moyo ya mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na jinsi jeshi la Myanmar linavyoamiliana na Waislamu wa Rohingya kwa hakika yanahesabiwa kuwa ni indhari na wakati huo huo yanatia wasiwasi mkubwa kuhusiana na mauaji ya kizazi na kukaririwa vitendo vya utumiaji mabavu dhidi ya binadamu yanayofanyika katika jimbo la Rakhine huko nchini Myanmar huku jumuiya zinazojulikana kama za kutetea haki za binadamu zikiwa zimefumbia jinai hizo.
Wanajeshi wa Myanmar kuanzia mwaka 1962 na wakiwa katika harakati za kuchukua hatamu za uongozi, walianzisha machafuko ya umwagaji damu dhidi ya Waislamu wa Rohingya.Jimbo la Rakhine lililoko magharibi mwa Myanmar ambalo hapo kabla likijulikana kwa jina la Arakan ni eneo la kijani kibichi, la misitu na lenye vituo vya uzalishaji na biashara nyingi na akthari ya wakazi wake ni Waislamu wa jamii ya Rohingya.
Jamii hiyo ambayo kwa mamia ya miaka imekuwa huko Rakhine ilisilimu baada ya kudhihiri Uislamu; na ukoo wa Salman Shah ulitawala katika eneo hilo kwa miaka 350 huku utawala huo ukiwa na sarafu yake maalumu ambayo juu yake ilikuwa imeandikwa Tawhidi yaani Kumpwekesha Mwenyezi Mungu. Baada ya wanajeshi kushika hatamu za uongozi nchini Myanamr walilidhibiti eneo hilo kwa shabaha ya kuwafukuza Waislamu kutoka katika makazi yao hayo. Jeshi la Myanmar liliwatangaza wakazi asili wa eneo hilo kuwa ni wahajiri wa Kibangladeshi na wakaanzisha hujuma dhidi yao.
Pamoja na kuwa katika kipindi cha ukoloni wa Uingereza kundi kutoka Bara Hindi ambapo Myanmar ilikuwa ikihesabiwa kuwa ni sehemu yake lilikimbilia katika jimbo la Rakhine kutokana na mateso ya Waingereza, lakini hii haina maana ya uhajiri wa jamii ya Rohingya katika eneo hili. Utumiaji mabavu na umwagaji damu ya Waislamu wa Rohingya ulishadidi na kushika kasi zaidi mwaka 1982 wakati waliponyimwa haki za kiraia na wanajeshi, ambapo mamia ya Waislamu wa Rohingya waliuawa kufuatia mashambulio ya wanajeshi na mabudha wenye kufurutu ada waliokuwa wakitaka kupora ardhi na nyumba zao.
Baadhi yao walikimbilia katika nchini jirani ikiwemo Bangladesh. Hatua ya jeshi la Myanmar ya kuwanyima haki ya uraia Waislamu wa jamii ya Rohingya kimsingi ilihalalisha mauaji ya kizazi na harakati za kuifuta jamii hiyo katika jimbo la Rakhine.
Kimya cha jamii ya kimataifa na watetezi eti wa haki za binadamu kwa hatua hizo za jeshi la Myanmar kiliwafanya wanajeshi hao waongeze mashambulio yao ya umwagaji damu dhidi ya Waislamu hao. Kwa msingi huo, matamshi ya mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na vitendo vya kinyama vya wanajeshi wa Myanmar ni ashirio la sehemu ndogo tu ya jinai ambazo zimekuwa zikifanyika kila siku nchini humo dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.
Hii ni katika hali ambayo, jumuiya za kimataifa zimekuwa zikitosheka na kutoa taarifa na indhari tu kwa serikali na wanajeshi wa Myanmar. Hata hivyo ukweli wa mambo katika nchi hiyo unaonyesha kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo sio tu hawazipi umuhimu indhari hizi, bali wamekuwa wakichuja mno habari na hivyo kuzuia kuripotiwa kama inavyotakiwa habari zinazohusiana na hali ya Waislamu wa Rohingya katika nchi hiyo.
Vyovyote itakavyokuwa, taarifa ya Yanghee Lee, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusiana na vitendo vya utumiaji mabavu na visivyo vya kibinadamu vya wanajeshi wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya inaiondolea kisingizio serikali ya nchi hiyo cha kuficha mambo au kusema uongo kuhusiana na tuhuma hizi na kwa sasa imeeleweka wazi kwa jamii ya kimataifa kwamba, mauaji ya Waislamu wa Rohingya na miamala isiyo ya kibinadamu dhidi yao ni harakati iliyoratibiwa na yenye malengo maalumu; hivyo ili kuzuia hali hiyo kuna udharura kwa Umoja wa Mataifa na jumuiya za kimataifa kuchukua hatua za dhati katika kukabiliana na vitendo hivyo.