UNICEF: Watoto zaidi ya 600 wameuawa nchini Syria 2016
Mfuko wa Kushughulikia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umesema mamia ya watoto waliuawa mwaka jana 2016 katika mgogoro wa Syria, mwaka unaotajwa kuwa mbaya zaidi kuuliwa watoto nchini humo.
Geert Cappelaere, Mkurugenzi wa UNICEF katika eneo la Mashariki ya Kati na eneo la Kaskazini mwa Afrika amesema kuwa, watoto 652 wameuawa katika mapigano na machafuko ya Syria mwaka uliopita 2016, kiwango ambacho ni sawa na ongezeko la asilimia 20 ukilinganisha na mwaka juzi 2015, ambapo watoto 255 waliuawa.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, akthari ya watoto hao waliuawa ama wakiwa madarasani au karibu na majengo ya shule na kwamba, mamilioni ya wengine wamelazimika kuitoroka nchi na sasa wanaishi kama wakimbizi katika nchi za Uturuki, Lebanon, Jordan, Misri na Iraq.
Ripoti ya Mfuko wa Kushughulikia Watoto wa Umoja wa Mataifa imesema kuwa, zaidi ya watoto milioni 6 wa Syria (sawa na ongezeko la asilimia 12 tokea mwaka 2012) kwa sasa wanategemea misaada ya kibinadamu.
Ripoti hiyo ya UNICEF imetolewa wiki moja baada ya shirika la Save the Children kutoa ripoti nyingine ya kuogofya iliyosema kuwa, asilimia 70 ya watoto wa Syria wanakabiliwa na msongo wa mawazo, ambao utaathiri mustakabali wao na vizazi vijavyo.