Korea Kusini yaishtaki China Shirika la Biashara Duniani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i26656-korea_kusini_yaishtaki_china_shirika_la_biashara_duniani
Waziri wa Biashara wa Korea Kusini Joo Hyung-hwan ametangaza kuwa nchi yake imewasilisha mashtaka dhidi ya China katika Shirika la Biashara Duniani (WTO) kutokana na vizuizi ilivyowekewa na Beijing katika sekta za biashara na utalii kulalamikia uwekaji mfumo wa makombora wa Marekani THAAD katika ardhi ya Korea Kusini.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 21, 2017 06:53 UTC
  • Korea Kusini yaishtaki China Shirika la Biashara Duniani

Waziri wa Biashara wa Korea Kusini Joo Hyung-hwan ametangaza kuwa nchi yake imewasilisha mashtaka dhidi ya China katika Shirika la Biashara Duniani (WTO) kutokana na vizuizi ilivyowekewa na Beijing katika sekta za biashara na utalii kulalamikia uwekaji mfumo wa makombora wa Marekani THAAD katika ardhi ya Korea Kusini.

Joo Hyung-hwan ameongeza kuwa katika mashtaka waliyowasilisha WTO wameeleza kuwa kuna uwezekano kwamba kwa hatua iliyochukua, China imekiuka baadhi ya makubaliano ya biashara.

Waziri wa Biashara wa Korea Kusini amefafanua kuwa mashtaka hayo yalifikishwa mbele ya mamlaka za Shirika la Biashara Duniani wiki iliyopita, baada ya China kuyawekea vizuizi kadhaa baadhi ya mashirika ya Korea Kusini katika sekta za utalii na masoko ya bidhaa.

Vizuizi vya kibiashara na kitalii vilivyowekwa na China dhidi ya mashirika ya Korea Kusini ambavyo vimeanza kutekelezwa baada ya kuidhinishwa rasmi uwekaji mfumo wa makombora wa Marekani wa THAAD katika ardhi ya Korea ya Kusini umeitia wasiwasi serikali ya Seoul kutokana na taathira zake hasi kwa uchumi wa nchi hiyo.

Waziri wa Biashara wa Korea Kusini, Joo Hyung-hwan

Malalamiko ya Seoul dhidi ya Beijing katika Shirika la Biashara Duniani yanaonyesha kuwa vizuizi vya kibiashara kwa uingizaji bidhaa za Korea Kusini nchini China pamoja na mashirika ya utalii ya nchi hiyo vimekuwa na taathira hasi kwa uchumi wa Seoul; na kuendelea kwa hali hiyo kunaweza kusababisha matatizo makubwa kwa mashirika ya korea Kusini yenye ushirikiano na Beijing.

Korea Kusini, ambayo iko kwenye orodha ya nchi zinazoongoza kiuchumi duniani inaitakidi kwamba, kuwa na nafasi athirifu kwenye soko kubwa la China ambalo ni soko kubwa zaidi la bidhaaa duniani kuna umuhimu mkubwa mno kwake; hivyo kupungua mgao wake katika soko la nchi hiyo kutakuwa na athari mbaya ambazo takriban haziweki kufidika katika masoko mengine mbadala.

Ni kwa sababu hiyo, ndiyo maana baada ya kukata tamaa ya kuwa na tija mashauriano ya kisiasa na kiuchumi waliyofanya kwa ajili ya kutenguliwa vizuizi vilivyowekwa na China, na kuhisi kwamba viongozi wa Beijing wamedhamiria kwa dhati kutekeleza maamuzi waliyopitisha, viongozi wa Korea Kusini wameamua kuwasilisha malalamiko yao kwenye Shirika la Biashara Duniani wakitaka suala hilo lichunguzwe na kuamuliwa na taasisi hiyo ya kimataifa ya biashara.

Pamoja na hayo, kauli ya Waziri wa Biashara wa Korea Kusini kwamba kuna uwezekano China imekiuka baadhi ya mikataba ya biashara inayosisitizwa na WTO kutokana na hatua yake ya kuiwekea vizuizi vya kiuchumi nchi hiyo inamaanisha kwamba Seoul haina uhakika kamili kama Beijing imekiuka mikataba hiyo.

Mfumo wa makombora wa THAAD

Katika kulalamikia uwekaji mfumo wa makombora wa Marekani THAAD katika ardhi ya Korea Kusini, Serikali ya China imetekeleza baadhi ya vizuizi vya kiuchumi dhidi ya nchi hiyo katika hali ambayo baada ya kuingizwa baadhi ya mitambo ya mfumo huo na kuainishwa tarehe ya mwisho ya kukamilishwa uwekaji mfumo huo ni baidi kwamba Korea Kusini itaghairi uamuzi wake kuhusiana na utekelezaji mradi huo.

Japokuwa mfumo wa makombora wa THAAD utawekwa hata kama China itaiwekea Korea Kusini vizuizi vya kiuchumi na kibiashara lakini yumkini Seoul ikalazimika kutoa baadhi ya upendeleo kwa Beijing ili ushirikiano baina ya nchi mbili urejee katika hali ya kawaida na kuondolewa vizuizi hivyo vilivyowekwa na China.

Mzozo baina ya China na Korea Kusini kuhusu uwekaji mfumo wa makombora wa THAAD wa Marekani umeonyesha kuwa kinyume na baadhi ya dhana zilizopo, China inazo nyenzo kadhaa inazoweza kuzitumia hususan katika sekta za uchumi ambayo ni injini ya ustawi wa Korea Kusini, zinazoweza kuisababishia Seoul matatizo makubwa…/