Ushirikiano na uelewa wa pamoja, dawa ya kuangamiza ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/world-i28178-ushirikiano_na_uelewa_wa_pamoja_dawa_ya_kuangamiza_ugaidi
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika makala iliyochapishwa kwenye gazeti la al Rai la Kuwait kwamba, njia pekee ya kupambana ipasavyo na ugaidi na misimamo ya kuchupa mipakai ni jamii ya kimataifa kufikia uelewa na ufahamu wa pamoja kwa ajili ya kuondoa tatizo hilo la dunia kote.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 24, 2017 03:27 UTC
  • Ushirikiano na uelewa wa pamoja, dawa ya kuangamiza ugaidi

Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika makala iliyochapishwa kwenye gazeti la al Rai la Kuwait kwamba, njia pekee ya kupambana ipasavyo na ugaidi na misimamo ya kuchupa mipakai ni jamii ya kimataifa kufikia uelewa na ufahamu wa pamoja kwa ajili ya kuondoa tatizo hilo la dunia kote.

Dakta Muhammad Javad Zarif ameeleza sababu za kuenea ugaidi katika maeneo mbalimbali ya dunia na kusema, ugaidi na misimamo ya kuchupa mipaka ni matokeo ya utendaji dhaifu na usiofaa wa jamii ya kimataifa na kwamba tatizo hilo si la Mashariki ya Kati pekee na wala halihusu dini au madhehebu maalumu.
Ugaidi na aina zake zite hauungwi mkono na dini yoyote ile, na dini zote na wafuasi wa dini hizo wanalaani harakati za kigaidi na makundi yenye fikra na misimamo yenye kufurutu mipaka. Hakuna dini yoyote duniani au wafuasi wa kweli wa dini ya mbinguni wanaounga mkono au kushabikia na kuhamasisha mauaji ya watu wasio na hatia, na dini zote hususan dini tukufu ya ya upendo na rehma ya Uislamu, zinasisitiza umuhimu wa wanadamu wote kuishi pamoja kwa amani na utulivu. 

Wingi wa makundi na madhehebu za kidini unatumiwa na maadui wa ubinadamu kuzusha mifarakano na hitilafu baina ya wanadamu ambao wamekuwa wakiishi kwa pamoja kwa amani na usalama kwa miaka mingi. Suala hilo limepelekea kujitokeza makundi mbalimbali ya kigaidi yanayotumia majina mbalimbali katika maeneo ya Asia, Afrika na kwengineko. Hapa inatupasa kuashiria kwamba, siasa za nchi za Magharibi kuhusu ugaidi haziko wazi na nchi hizo zinachangia kueneza ugaidi zaidi katika kona mbalimbali za dunia kwa kushindwa kuwa na maana moja kuhusu janga hilo. 

Magaidi wa Daesh wanaungwa mkono na Marekani

Katika upande mwingine, jumuiya na taasisi za kimataifa zimeathiriwa sana na madola makubwa na kushindwa kuwa na mchango wa maana katika kukabiliana na uovu huo. Nchi hizo za Magharibi zinautumia ugaidi kama wenzo wa kutimizia malengo na matakwa yao, suala ambalo limeifanya jamii ya kimataifa ishindwe kuwa na sera moja ya kupambana na ugaidi.

Sera na misimamo hiyo ya nchi kubwa hususan za Magharibi kuhusu ugaidi zinachukuliwa wakati hii leo janga hilo limekuwa maumivu na tatizo linalousumbua ulimwengu na wanadamu wote wa mashariki na magharibi mwa dunia. Ugaidi ambao unajulikana hii leo kwa jina la Daesh (ISIS) na ambao umekuwa ukiwatesa watu wasio na hatia wa Iraq na Syria kwa miaka kadhaa, sasa umeingia katika miji mikuu ya nchi za Ulaya. Suala hilo linaonesha kuwa, tatizo la ugaidi halihusu eneo, mbari, dini wala madhehebu makhsusi. Katika mazingira kama hayo, ni uelewa wa pamoja na ushirikiano wa pande zote tu ndio unaoweza kuisaidia jamii ya kimataifa kukabiliana ipasavyo na janga hilo. 

Jambo jingine linalipaswa kusisitizwa hapa ni kuwa, mapambano dhidi ya ugaidi hayapaswi kuhusu njia za kijeshi na kiusalama pekee, bali kuna udharura wa kutumia mbinu za kiutamaduni, kijami na kiuchumi katika juhudi za kukabiliana na janga hilo ambalo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikiikumbusha jamii ya kimataifa kuhusu balaa la ugaidi na mwaka 2013 Rais Hassan Rouhani alihutubuia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kutoa pendekezo la kuwepo ulimwengu usio na ugaidi na misimo ya kuchupa mipaka ambalo lilipasishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.