Jun 18, 2017 13:45 UTC
  • Mkasa wa moto msituni waua watu 58 nchini Ureno

Habari kutoka Ureno zinasema watu 58 wamethibitishwa kufariki dunia baada ya moto mkubwa ulioanzia katika msitu mmoja uliko karibu na mji wa Pedrogao Grande, katikati mwa nchi kuteketeza magari na makazi ya watu.

Jorge Gomes, afisa katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi ameliambia shirika la habari la AP kuwa, mbali na vifo hivyo, watu 60 wakiwemo wazima moto wanne na mtoto mdogo wamepata majeraha mabaya ya kuungua kutokana na mkasa huo.

Duru za polisi zinasema moto huo unaaminika kuanzishwa na umeme na 'radi kavu' vilivyopiga msitu mmoja katika eneo la Pedrogao Grande, ambapo ulisambaa na kuenea katika makazi ya watu yaliyoko karibu na mji huo.

Moto huo ukiteketeza makazi ya watu

Habari zaidi zinasema kuwa, aghalabu ya watu waliopoteza maisha kutokana na mkasa huo ni watu waliokuwa ndani ya magari yao wakijaribu kuukimbia moto huo mjini Pedrogao Grande, yapata kilomita 50 kusini mashariki mwa mji wa Coimbra.

Meya wa mji huo Valdemar Alves amesema ingawa visa vya moto kuteketeza misitu vimekuwa vikishuhudia katika eneo hilo, lakini idadi ya vifo mara hii ni ya kushtua. 

Takriban wazima moto 700 wanaendeleza jitihada za kuuzima moto huo tangu jana Jumamosi.

Tags