Ufaransa na mgogoro wa wakimbizi wa Calais
https://parstoday.ir/sw/news/world-i32660-ufaransa_na_mgogoro_wa_wakimbizi_wa_calais
Mamia ya wakimbizi walioko katika kambi ya Calais huko kaskazini mwa Ufaransa wanaendelea kusumbuliwa na hali mbaya kupita kiasi, na siasa na sera tofauti na zinazokinzana za viongozi wa Ufaransa zimezidisha hali mbaya ya wakimbizi hao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 03, 2017 21:56 UTC
  • Ufaransa na mgogoro wa wakimbizi wa Calais

Mamia ya wakimbizi walioko katika kambi ya Calais huko kaskazini mwa Ufaransa wanaendelea kusumbuliwa na hali mbaya kupita kiasi, na siasa na sera tofauti na zinazokinzana za viongozi wa Ufaransa zimezidisha hali mbaya ya wakimbizi hao.

Baada ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa kutoa wito usio wa kibinadamu ikiitaka serikali kukata huduma za maji ya kunywa na afya kwa wakimbizi walioko katika eneo la Calais, Baraza la Serikali ya Paris ambalo ndio marejeo ya juu zaidi ya mahakama za nchi hiyo imesema kuwa, hali ya wakimbizi wa eneo hilo haikubaliki na kusisitiza kuwa, takwa la kukatwa huduma za maji na afya kwa wakimbizi hao lililotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani si la kisheria na kwamba mienendo ya dola dhidi ya wakimbizi hao si ya kibinadamu.

Wakimbizi katika mji wa Calais, Ufaransa

Mji wa Calais ulioko kaskazini mwa Ufaransa una bandari yenye shughuli nyingi zaidi katika njia ya baharini inayoitwa na Waingereza kwa jina la English Channel wakati Wafaransa wakiita La Manche. Eneo hilo lina mamia ya wakimbizi wanaofanya mikakati ya kuelekea Uingereza kwa matarajio ya kupata maisha bora zaidi. Tangu maafisa wa Ufaransa walipowafukuza wakimbizi karibu elfu 9 katika eneo la msitu wa Calais katika kipindi cha mapukutiko cha mwaka jana wa 2016, serikali kuu ya Ufaransa na tawala za kieneno zinafanya jitihada kubwa kuhakikisha kwa njia yoyote ile kwamba, wakimbizi hawakusanyiki tena katika eneo hilo. Kwa kadiri kwamba, serikali imekata kabisa suhula na huduma zote muhimu kwa ajili ya wakimbizi hao kama maji, chakula na tiba. Si hayo tu bali askari usalama na polisi wamepewa jukumu la kuwafurusha na kuwafuatilia wakimbizi katika eneo hilo. 

Wakimbizi wa Calais wakifurushwa na polisi ya Ufaransa

Mwanaharakati wa haki za binadamu wa Ufaransa, Benedict Genarado, anasema kuhusu kadhia hiyo kwamba: "Hali ya wakimbizi katika kambi ya Calais ni ya maafa na kuna udharura wa kushughulikiwa hali hiyo haraka iwezekanavyo. Kuna nyaraka na ushahidi wa kutosha unaothibitisha kuwa polisi ya Ufaransa inaamiliana na wakimbizi hao kwa mwenendo mbaya. Nyaraka hizo zinaonesha kuwa, polisi inatumia mabavu dhidi ya watu wasio na uwezo wowote", mwisho wa kunukuu.

Serikali ya Ufaransa pia inakwamisha na kutatiza shughuli za mashirika na jumuiya zisizo za serikali zinazowasaidia wakimbizi na inazuia harakati za kufikishwa misaada kwa wakimbizi hao.

Hatua hizo za serikali ya Ufaransa dhidi ya wahajiri na ukiukaji wake mkubwa wa haki muhimu zaidi ya uhuru wa binadamu unashuhudiwa wakati huu ambapo wachambuzi wengi wa mambo wanasisitiza kuwa, mgogoro wa wakimbizi barani Ulaya ni matokeo ya sera na siasa za nchi za bara hilo za kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Siasa hizo zinatekelezwa na Marekani, nchi za Ulaya na washirika wao wa Kiarabu. Matokeo ya siasa hizo ni ghasia na machafuko makubwa yanayoshuhudiwa katika baadhi ya nchi za mashariki mwa Asia na kaskazini mwa Afrika ambayo yamesababisha wimbi kubwa la wakimbizi kuelekea Ulaya.

Ukweli ni kuwa, mienendo isiyo ya kibinadamu ya maafisa wa Ufaransa imeweka wazi zaidi siasa na sura halisi ya nchi za Magharibi zinazodai kubeba bendera ya kutetea haki za binadamu.