Kuendelea jinai dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar
Idadi kadhaa ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wamefariki dunia katika Mto Naf katika mpaka wa Myanmar na Bangladesh walipokuwa wakikimbia ukandamizaji unaofanywa na wanajeshi wa serikali ya nchi hiyo dhidi ya jamii hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya kikosi cha ulinzi wa mpakani cha Bangladesh, kwa akali watoto 11 na wanawake 15 Waislamu wa Myanmar wamefariki dunia katika tukio hilo. Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, zaidi ya nyumba 2600 za Waislamu wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine lililoko magharibi mwa Myanmar zimechomwa moto na jeshi la nchi hiyo.
Ripoti ya Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) inaonyesha kuwa, takribani Waislamu elfu sitini wa Kirohingya wamekimbilia nchini Bangladesh baada ya kushadidi mauaji na vitendo vya ukandamizaji dhidi yao. Duru mpya ya vitendo vya utumiaji mabavu na mauaji dhidi ya Waislamu wa Kirohingya ilianza baada ya jeshi la Myanmar kupeleka kikosi katika jimbo la Rakhine la magharibi mwa nchi hiyo.
Licha ya malalamiko ya duru za kisiasa kuhusiana na matokeo mabaya ya kutumwa jeshi huko Rakhine, lakini serikali ya Myanmar ilidai kuwa, kikosi hicho kimetumwa huko ili kudhamini usalama na kuwalinda Waislamu hao. Hii ni katika hali ambayo, ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, wanajeshi wa Myanmar wamekuwa wakihusika moja kwa moja na mauaji dhidi ya Waislamu hao.
Ripoti mbalimbali za kuaminika zinaonyesha kuwa, baadhi ya Waislamu wa Rohingya wamekuwa wakiuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi hao au kupitia hujuma ya mabudha wenye misimamo ya kufurutu ada ambao nao wamekuwa wakipata himaya ya jeshi.
Aidha Waislamu wa Rohingya wamekuwa wakipoteza maisha kwa kuzama boti wanazosafiria wakikimbia hujuma za mabudha na wengine hufa kwa njaa wakiwa njiani huku baadhi yao wakitangatanga katika misitu na baharini wakiwa katika juhudi za kukimbia vitendo vya utumiaji mabavu vinavyowalenga.
Hii ni katika hali ambayo, baada ya kufanyika marekebisho ya kisiasa na kiuchumi nchini Myanmar walimwengu walikuwa wakitaraji kwamba, serikali ya nchi hiyo itachukua hatua ya kulipatia ufumbuzi tatizio la Waislamu wa Rohingya.
Kwani kimsingi hatua ya serikali ya Myanmar ya kuwanyima haki ya uraia Waislamu hao ndio iliyoandaa uwanja wa mauaji na vitendo vya kinyama dhidi yao.
Marie Lall, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Heidelberg cha nchini Ujerumani na mtaalamu wa masuala ya Myanmar anasema: Baada ya kufanyika marekebisho ya kiuchumi na kisiasa nchini Myanmar, licha ya kuwa hali ya kifedha ya watu katika miji imeboreka, lakini faida ya hilo sio tu kwamba, na haiyafikii maeneo ya vijijini na viunga vyake, bali hali hii imezidisha mazingira magumu kwa akthari ya jamii za waliowachache kuweza kumiliki nyumba na makazi.
Ramzy Baroud mwandishi wa habari Mmarekani mwenye asili ya Palestina ambaye anaishi Washington anasema: Baada ya Myanmar kuondolewa vikwazo, ulimwengu wa Magharibi ulipata fursa mwafaka ya kunufaika na vyanzo vya utajiri vya nchi hiyo na hili ni jambo ambalo linapewa kipaumbe na madola ya Magharibi kuliko hata suala la haki za binadamu. Ni kwa mintarafu hiyo ndio maana madola hayo yamenyamazia kimya mauaji dhidi ya Waislamu wa Myanmar na yanachokifuatilia katika nchi hiyo ni maslahi yao ya kiuchumi tu.
Vyovyote itakavyokuwa, inavyoonekana ni kuwa, nchi na asasi za Kiislamu ndizo zinazoweza kuchukua hatua za maana za kuhitimisha jinai za jeshi la Myanmar na mabudha wenye misimamo mikali dhidi ya Walislamu wa Rohingya. Indonesia na Malaysia zikiwa nchi za Kiislamu wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini na Mashariki mwa Asia ambapo Myanmar pia ni mwanachama katika jumuiya hiyo, zina jukumu zito zaidi la kuzuia unyama na ukatili dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya.