Mauaji ya Waislamu wa Rohingya ni njama iliyoratibiwa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34063-mauaji_ya_waislamu_wa_rohingya_ni_njama_iliyoratibiwa
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH) limetoa taarifa na kusema kuwa, mauaji ya hivi sasa ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar na hatua ya mashirika ya kutetea haki za binadamu ya kupuuza ukatili huo ni jambo linaloashiria njama iliyoratibiwa tangu zamani dhidi ya Waislamu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 08, 2017 07:01 UTC
  • Mauaji ya Waislamu wa Rohingya ni njama iliyoratibiwa

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH) limetoa taarifa na kusema kuwa, mauaji ya hivi sasa ya Waislamu wa jamii ya Rohingya nchini Myanmar na hatua ya mashirika ya kutetea haki za binadamu ya kupuuza ukatili huo ni jambo linaloashiria njama iliyoratibiwa tangu zamani dhidi ya Waislamu.

Katika taarifa yake hiyo, jeshi hilo limesema: "Jinai za kuogofya zinazofanywa na Mabudhha wenye misimamo mikali na Jeshi la Myanmar dhidi ya Waislamu ni jambo linaloashiria kuweko njama zinazotekelezwa kwa mpangilio maalumu dhidi ya Uislamu. Iwapo jinai hii haitasitishwa basi kutashuhudiwa mauaji mengine ya halaiki katika historia ya mwanadamu."

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia limelaani undumakuwili wa wale wanaodai kuwa ni watetezi wa haki za binadamu ambao wamepuuza mauaji ya Waislamu wa Rohingya. Aidha jeshi hilo limetoa wito kwa mataifa yote duniani yachukue jukumu la kuwasaidia Waislamu wanaodhulumiwa Myanmar.

Wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya

Taarifa hiyo pia imeitaka serikali ya Iran kutumia uwezo wake wote kuwanusuru Waislamu wa Myanmar. Huku hayo yakijiri, taarifa zinasema Mabudhha wenye misimamo mikali wanaendelea kutetekteza kwa moto vijiji vya Waislamu katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar.

Ijumaa ya tarehe 25 Agosti lilianza wimbi jipya la mashambulizi ya kikatili ya jeshi la Myanmar na Mabudha dhidi ya Waislamu wasio na ulinzi wa Rohingya katika mkoa wa Rakhine wa magharibi mwa Myanmar ambapo duru zinasema hadi sasa mamia ya Waislamu wameangamizwa kwa umati. Halikadhalika tangu wakati huo hadi hivi sasa zaidi ya Waislamu laki moja na 70 elfu wamekimbia makazi yao.

Mwaka 2012 jeshi la Myanmar lilianzisha mashambulizi mapya ya kikatili dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya na hadi hivi sasa serikali ya mabudha ya nchi hiyo inawanyima Waislamu hao haki zao za kimsingi kabisa kama vile uraia.