Wananchi wa Marekani wanapinga kushambuliwa kijeshi Korea ya Kaskazini
Uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni nchini Marekani unaonyesha kuwa aghalabu ya wananchi wanapinga kushambuliwa kijeshi Korea ya Kaskazini.
Gazeti la Washington Post limeripoti kuwa uchunguzi mpya wa maoni wa hivi karibuni unaonyesha kuwa asilimia 67 ya wananchi wa Marekani wanapinga shambulio la kijeshi dhidi ya Korea ya Kaskazini. Uchunguzi huo wa maoni aidha umeonyesha kuwa wananchi wa Marekani wana imani zaidi na viongozi wa kijeshi kuliko Rais wao Donald Trump katika kuamiliana na kadhia ya nyuklia ya Korea ya Kaskazini licha ya kupinga kushambuliwa kijeshi nchi hiyo. Rais wa Marekani kwa mara kadhaa sasa ametishia kuishambulia kijeshi Korea ya Kaskazini.
Tafiti nyingine za maoni zilizofanywa huko Marekani zinaonyesha kuwa ni asilimia 39 pekee ya wananchi wa Marekani ndio wanaafiki utendaji wa Trump ikiwa imepita miezi minane tangu kushika hatamu za uongozi nchini humo. Hali ya mvutano imeongezeka katika wiki za hivi karibuni kati ya Marekani na Korea ya Kaskazini kufuatia matamshi ya vitisho ya Trump kutaka kuishambulia kijeshi nchi hiyo.