Korea Kaskazini: Marekani ndio iliyoanzisha mchezo wa nyuklia, tutakabiliana nayo
Afisa wa ngazi ya juu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini amesema kuwa, Pyongyang itaendelea kujiimarisha zaidi kwa silaha za nyuklia kwa ajili ya kukabiliana na vitisho vya Marekani.
Nam Hyok-Tsen, wa Kitengo cha Utafiti wa Masuala ya Marekani katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Korea Kaskazini ameyasema hayo katika kikao cha kimataifa cha kuangamiza silaha za nyuklia mjini Moscow, mji mkuu wa Russia. Akibainisha kwamba Marekani ndiyo iliyoanzisha mchezo wa silaha za nyuklia amesema kuwa, Pyongyang itaendelea kuzifanyia majaribio silaha zake za nyuklia.
Kabla ya hapo pia Naibu Spika wa Bunge la Korea Kaskazini akizungumza katika kikao cha 137 cha Umoja wa Mabunge ya Dunia (IPU) kilichofanyika mjini Saint Petersburg, Russia alisema kuwa, Pyongyang inahitajia silaha za nyuklia kwa ajili ya kukabiliana na vitisho vya Marekani. An Tong Chun alifafanua kuwa, kustawishwa silaha za nyuklia na makombora ya balestiki ni miongoni mwa masuala yenye kuzingatiwa na Korea Kaskazini. Mvutano kati ya Washington na Pyongyan ulishtadi baada ya kuingia madarakani Rais Donald Trump nchini Marekani.
Hii ni kwa kuwa mara kadhaa Trump ametishia kuishambulia kijeshi nchi hiyo ya Asia, suala ambalo limeifanya Pyongyang nayo kujibu vitisho hivyo. Sambamba na Washington kushadidisha mgogoro katika eneo la Peninsula ya Korea, imekuwa ikiitaka Korea Kaskazini pia kusitisha miradi yake ya silaha za nyuklia na makombora ya balestiki.