Rais wa zamani wa Marekani akosolewa kwa kumdhalilisha kijinsia mwanamke
Rais wa zamani wa Marekani 'ameomba msamaha' baada ya kukosolewa vikali na duru mbali mbali kwa kumfanyia ukatili wa kijinsia na unyanyasaji wa kingono muigizaji wa filamu mwenye umri wa miaka 34.
Mwanamke huyo kwa jina Heather Lind ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandano wa kijamii wa Instagram kwamba, George Bush mwenye umri wa miaka 93 alimdhalilisha na kumkosea heshima kwa kumgusa sehemu yake ya makalio.
Amesema tukio hilo lilfanyika miaka minne iliyopita, katika tamasha la kuipigia debe filamu yenye anwani "Turn: Washington's Spies."
Mcheza filamu huyo wa Marekani ameandika: "Wakati tuliposimama kupigwa picha, George Bush ambaye alikuwa ameketi kwenye kiti cha magurudumu akiwa pamoja na mkewe Barbara Bush alinifanyia ukatili wa kijinsia kwa kunitomasa sehemu zangu za makalio, huku akininong'onezea maneno machafu masikioni."
Msemaji wa familia ya Bush hata hivyo amesema rais huyo wa Marekani tayari ameomba radhi na kusisitiza kuwa, huo ulikuwa utani na maneno aliyomwambia mwanamke huyo ni ya kawaida ambayo amekuwa akiyasema mara kwa mara ili kuleta ucheshi.
Hii ni katika hali ambayo, waigizaji na wacheza filamu za Hollywood wameanzisha kampeni za kufichua wahusika wa kashfa za ufuska katika tasnia hiyo, kwenye mitandao ya kijamii.
Hii ni baada ya gazeti la New York Times mapema mwezi huu kuchapisha matokeo ya uchunguzi wao kuhusu moja kati ya vinara wa sekta ya filamu ya Hollywood, Harvey Weinstein, anayetuhumiwa kuwadhalilisha kijinsia makumi ya waigizaji wa Hollywood.