Waziri wa Uingereza ajiuzulu kwa kufanya mikutano ya siri na Netanyahu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i36270-waziri_wa_uingereza_ajiuzulu_kwa_kufanya_mikutano_ya_siri_na_netanyahu
Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Priti Patel amelazimika kujiuzulu kutokana na mtikisiko wa kisiasa nchini humo uliosababishwa na yeye kufanya mikutano ya siri na maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel akiwemo Waziri Mkuu wa utawala huo bandia, Benjamin Netanyahu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 09, 2017 04:20 UTC
  • Waziri wa Uingereza ajiuzulu kwa kufanya mikutano ya siri na Netanyahu

Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Priti Patel amelazimika kujiuzulu kutokana na mtikisiko wa kisiasa nchini humo uliosababishwa na yeye kufanya mikutano ya siri na maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel akiwemo Waziri Mkuu wa utawala huo bandia, Benjamin Netanyahu.

Waziri huyo ambaye alikuwa katika ziara ya kikazi nchini Kenya ameagizwa kurejea nchini Uingereza na Waziri Mkuu, Theresa May, baada ya kufichuka kuwa alifanya vikao 12 na maafisa wa ngazi za juu wa Israel pamoja na wakuu wa mashirika kadhaa ya utawala huo wakati alipokuwa likizo ya kifamilia mwezi Agosti mwaka huu.

Kitendo hicho cha Priti Patel kimetajwa na wadadisi wa mambo kama ukiukaji mkubwa wa itifaki ya kidiplomasia. May alilazimika kukatiza safari ya Patel barani Afrika, baada ya duru za habari kufichua kuwa, waziri huyo wa Uingereza alifanya vikao vingine vya siri na wanasiasa wa Israel mwezi Septemba mwaka huu, sanjari na kutembelea Miinuko ya Golan nchini Syria, ambayo imekaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel toka mwaka 1967.

Theresa May

Katika barua yake ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Theresa May, Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza amesema kuwa: "Licha ya kuwa kitendo changu hicho kilikuwa na nia njema, lakini kilikosa uwazi, jambo ambalo nimekuwa nikilipigania kwa muda mrefu. Kwa mantiki hiyo, naomba radhi kwako na kwa serikali, na naomba kujiuzulu."

Theresa May amekubali ombi la waziri huyo kujiuzulu na kusema kuwa ni hatua nzuri inayoonyesha kiwango cha juu cha uwazi ambao waziri huyo amekuwa akishinikiza.