Russia: Uchunguzi ufanyike kuhusu shambulizi la anga la Marekani Kunduz, Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/world-i36332-russia_uchunguzi_ufanyike_kuhusu_shambulizi_la_anga_la_marekani_kunduz_afghanistan
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imewataka maafisa wa serikali ya Afghanistan na taasisi za kimaraifa za kutetea haki za binadamu wafanye uchunguzi kamili na usiopendelea upande wowote kuhusu shambulizi la anga la Marekani katika mji wa Kunduz nchini Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 12, 2017 01:04 UTC
  • Russia: Uchunguzi ufanyike kuhusu shambulizi la anga la Marekani Kunduz, Afghanistan

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imewataka maafisa wa serikali ya Afghanistan na taasisi za kimaraifa za kutetea haki za binadamu wafanye uchunguzi kamili na usiopendelea upande wowote kuhusu shambulizi la anga la Marekani katika mji wa Kunduz nchini Afghanistan.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia pia imetoa wito wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kuzuia kukaririwa mashambulizi ya ndege za kivita za Marekani katika maeneo mbalimbali ya Afghanistan.

Tarehe 3 mwezi huu wa Novemba ndege za kivita za Marekani zilishambulia eneo la Char Dara katika mkoa wa Kunduz nchini Afghanistan na kuua karibu raia 55. Raia wengine wengi pia walijeruhiwa katika shambulizi hilo.

Novemba mwaka 2015 pia ndege za kivita za Marekani zilishambulia hospitali iliyokuwa ikisimamiwa na Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mpaka katika mji huo huo wa Kunduzi na kuua madaktari na wagonjwa na 42 waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo. Makumi ya raia wengine walijeruhiwa.

Wahanga wa mashambulizi ya Marekani, Afghanistan

Mashambulizi hayo ya Marekani yanakiuka mkataba wa amani wa Washington na Kabul ambayo Marekani iliahidi kutoshambulia maeneo ya raia. 

Maelfu ya raia wa Afghanistan wameuawa katika mashambulizi yanayoendelea kufanywa na Marekani nchini humo tangu Washington ilipotuma majeshi yake huko Afghanistan mwaka 2001 kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi.