Nov 15, 2017 07:45 UTC
  • Imarati yazitaka nchi za Ulaya zidhibiti misikiti kwa kuweka CCTV

Waziri mmoja wa Umoja wa Falme za Kiarabu UAE ameitaka Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya kudhibiti misikiti na makhatibu wa misikiti katika nchi zao kwa shabaha ya kuzuia uenezwaji wa misimamo mikali ya kufurutu ada.

Sheikh Nahyan bin Mubarak Al-Nahyan ameliambia shirika la habari la DPA la Ujerumani kuwa: "Hamuwezi kuacha wazi milango ya misikiti kwa yeyote kuingia atakavyo, na kuacha mtu yeyote ahubirie hadhira kwenye misikiti hiyo."

Waziri huyo wa Imarati amesema nchi za Ulaya sharti ziiweke misikiti ya nchi zao chini ya uangalizi wa kamera za CCTV, sambamba na kuwadhibiti wanaotoa hotuba katika misikiti hiyo ili kupambana na ueneaji wa misimamo iliyochupa mipaka,

Waislamu wa Ujerumani

Hii ni katika hali ambayo, mwezi Agosti mwaka huu, Qatar ilifichua nyaraka zinazoonyesha kuwa Saudi Arabia na Imarati zinawaunga mkono magaidi wa mtandao wa al-Qaeda na kundi la kitakfiri la Daesh (ISIS) nchini Yemen.

Televisheni ya Aljazeera ya Qatar ilifichua nyaraka mpya zilizotolewa na wataalamu wa kamati ya vikwazo ya Umoja wa Mataifa dhidi ya nchi hizo mbili zinazoonyesha kuwa tawala za Riyadh na Abu Dhabi zinayafadhili kifedha makundi ya kitakfiri likiwemo la al-Qaeda kusini mwa Yemen.

Tags