UN: Myanmar sio salama kwa Waislamu Warohingya kurejea
https://parstoday.ir/sw/news/world-i36743-un_myanmar_sio_salama_kwa_waislamu_warohingya_kurejea
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema hali katika mkoa wa Rakhine nchini Myanmar sio shwari kuweza kuwapokea malaki ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbilia nchini Bangladesh.
(last modified 2026-02-18T07:37:01+00:00 )
Nov 24, 2017 15:52 UTC
  • UN: Myanmar sio salama kwa Waislamu Warohingya kurejea

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR limesema hali katika mkoa wa Rakhine nchini Myanmar sio shwari kuweza kuwapokea malaki ya wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya waliokimbilia nchini Bangladesh.

Katika taarifa iliyotolewa leo Ijumaa na UNHCR, shirika hilo la wakimbizi limesema halijaona maelezo kuhusu makubaliano yaliyofikiwa kati ya Bangladesh na Myanmar ya kurejea nyumbani wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa, sio wakati mwafaka wa kuwarejesha wakimbizi hao nchini Myanmar, kwani wakati huu kuna wakimbizi wengine wanaoendelea kuukimbia mkoa wa Rakhine kutokana na kutendewa jinai mbali mbali kama vile kubakwa.

Nyumba za Waislamu wa Mynmar zilizoteketezwa moto mkoani Rakhine

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema ni mapema mno kuwarejesha wakimbizi hao nyumbani wakati ambapo aghalabu yao wangali wana makovu na msongo wa mawazo kutokana na jinai walizofanyiwa wao au jamaa zao, na kwamba hawana pa kurejea kwa kuwa vijiji vyao viliteketezwa moto.

Hii ni katika hali ambayo, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema kuwa, kutiwa saini makubaliano kati ya nchi hizo kuhusiana na kurejea nchini kwao wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya ni hatua muhimu katika jitihada za kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tangu tarehe 25 Agosti mwaka huu hadi sasa. Mauaji hayo ya umati dhidi ya Waislamu nchini Myanmar yamepelekea zaidi ya nusu milioni kati yao kukimbilia hifadhi katika nchi jirani ya Bangladesh.

Wanajeshi wa Myanmar wanashirikiana na Mabudha kuwaua na kuwatesa Waislamu wa Rohingya