Bunge la EU lataka Saudia iwekewe vikwazo vya silaha
Wabunge wa Umoja wa Ulaya wamepiga kura kwa kishindo kuunga mkono azimio linalotaka EU iiwekee vikwazo vya silaha Saudi Arabia, inayoongoza katika mauaji na hujuma za kijeshi dhidi ya Yemen.
Wabunge 539 jana Alkhamisi walipiga kura ya ndio kuunga mkono azimio hilo, huku 13 pekee wakipinga. Wabunge hao wa EU wameyataja mashambulizi ya Saudia na waitifaki wake dhidi ya raia wasio na hatia wa Yemen kuwa jina za kivita.
Kadhalika wabunge hao wa Umoja wa Ulaya wamezijia juu nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, kwa kuruhusu kuendelea kuuziwa silaha Saudia, hatua wanayosema inakiuka sheria ya kudhibiti mauzo ya silaha ya EU.
Uingereza, Ufaransa, Ugiriki na Ujerumani ni miogoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya zilizofunga mkataba wa mauzo ya silaha na Saudia, tangu Riyadh ianzishe hujuma zake dhidi ya nchi hiyo maskini jirani yake mwaka 2015.
Mwaka jana, Ufaransa iliiuzia Saudia silaha zenye thamani ya dola bilioni 18 za Marekani, huku Marekani ikitajwa kuwa muuzaji wa pili mkubwa wa silaha kwa Riyadh, ambapo imeiuzia silaha zenye thamani ya dola bilioni 5.9, ikifuatiwa na Uingereza, zaidi ya dola bilioni 4.
Saudia kwa uungaji mkono wa Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel, Imarati na baadhi ya nchi za Kiarabu, ilianzisha mashambulizi ya kikatili ya pande zote dhidi ya wananchi wa Yemen mwezi Machi 2015, ambapo watu zaidi ya 12 elfu wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa.