Taarifa ya OIC ya kulaani uamuzi wa Marekani kuhusu Baytul Muqaddas
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imeonyesha kusikitishwa kwake na uamuzi wa Rais Donald Trump wa Marekani wa kuutangaza mji mtakatifu wa Quds wenye Kibla cha Kwanza cha Waislamu kuwa eti ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Taarifa ya OIC imeeleza kuwa, agizo la Trump la kuhamishiwa ubalozi wa Marekani huko Baytul Muqqas kutoka Tel Aviv ni kuzivunjia heshima hisia za Waislamu na kwamba, hatua hiyo inakinzana wazi na sheria pamoja na maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Sehemu moja ya taarifa ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imesema: Hatua ya Marekani ya kuutangaza mji wa Quds kuwa mji mkuu wa Israel, inadhoofisha nafasi ya Marekani kama msimamizi wa amani.
Aidha OIC imetoa wito wa kufanyika haraka iwezekanavyo kikao cha nchi wanachama wa jumuiya hiyo hapo tarehe 12 na 13 mwezi huu kwa ajili ya kujadili uamuzi huo wa Marekani na kuchukua msimamo mmoja kwa ajili ya kukabiliana na hatua hiyo ya dharua ya Donald Trump.
Katika sehemu nyingine ya taarifa hiyo, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imeitaja hatua hiyo kwamba, si tu ni tishio kwa utambulisho wa Waislamu bali kwa Wakristo pia na mahusiano ya milele ya Waislamu na Masjidul Aqswa kikiwa kitovu cha kadhia ya Palestina.
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC imeitaka jamii ya kimataifa kutoa ushirikiano unaohitajika kwa ajili ya kukabiliana na uamuzi huo wa Rais Donald Trump wa Marekani.