Marekani iko tayari Bashar Assad aendelee kubakia madarakani hadi mwaka 2021
Ripoti za baadhi ya duru za habari nchini Marekani zinaeleza kuwa baada ya kukata tamaa ya kumwondoa madarakani Rais Bashar Al Assad wa Syria, serikali ya Washington imechukua uamuzi mpya wa kuafiki Assad aendelee kuwa rais wa Syria hadi mwaka 2021.
Kwa mujibu wa gazeti la The New Yorker, Rais Donald Trump wa Marekani yuko tayari kukubali Rais Bashar Al Assad aendelee kubaki madarakani hadi mwaka 2021.
Hii ni katika hali ambayo mnamo mwezi Oktoba mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson alidai kuwa enzi za utawala wa ukoo wa Assad zinakaribia ukingoni na kusisitiza kuwa "Marekani inataka Syria ibaki kuwa nchi moja kamili iliyoungana na Bashar Al Assad asiwe na nafasi yoyote katika serikali ya nchi hiyo".
Kwa mujibu wa ripoti ya The New Yorker, uamuzi mpya wa Marekani unaonyesha machaguo haba iliyobaki nayo serikali ya Marekani, ukweli halisi wa hali ya nguvu za kijeshi ilivyo nchini Syria na mafanikio ziliyopata Russia, Iran na Hizbullah katika kuilinda serikali ya Assad.
Gazeti hilo limeendelea kueleza kuwa Washington imewekwa kando kidiplomasia na pande tatu zenye nguvu ambazo ni Russia, Iran na Uturuki ambazo ndizo zilizoshika hatamu za mchakato wa amani wa Syria.
Katika kipindi cha miaka saba iliyopita, Marekani imeyasaidia pakubwa kwa fedha na silaha, kijeshi na kisiasa na kwa propaganda za vyombo vya habari makundi ya wapinzani na ya magaidi kwa lengo la kuuangusha mfumo wa utawala wa Syria; hata hivyo imegonga mwamba na kushindwa kufikia lengo lake hilo.../