UN: Huenda Suu Kyi akafunguliwa mashitaka ya mauaji ya kimbari
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema uhalifu unaofanywa na wanajeshi wakishirikiana na Mabudha nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ni mauaji ya kimbari na yumkini wanaohusika wakiwemo viongozi wa nchi hiyo wakapandishwa kizimbani karibuni hivi.
Zeid Ra'ad al-Hussein amesema jinai hizo dhidi ya Warohingya zinafanyika kwa utaratibu na mpangilio maalumu akisisitiza kuwa, binafsi alimpigia simu Aung San Suu Kyi, Waziri wa Mambo ya Nje na Mshauri Mkuu wa serikali ya nchi hiyo akimtaka asitishe operesheni za kijeshi dhidi ya Waislamu hao ambao ni miongoni mwa jamii za watu walio wachache nchini humo.
Afisa huyo wa UN amesema aliwasiliana na Suu Kyi hata kabla ya kuanza wimbi la kwanza la operesheni hizo za kikatili mnamo Januari mwaka huu.
Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa tangu kuanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo tarehe 25 Agosti mwaka huu.
Kwa mujibu wa shirika la Madaktari Wasio na Mipaka, zaidi ya Waislamu 6,700 wa Rohingya waliuawa ndani ya mwezi mmoja tangu wimbi jipya la ukatili wa wanajeshi wakishirikiana na Mabudha lianze.
Kadhalika shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema jeshi la Myanmar linawaua kiholela na kuwanajisi wanawake Waislamu wa jamii ya Rohingya magharibi mwa nchi hiyo.