Viongozi wa kisiasa Pakistan wakerwa na Trump, waitaka serikali kuisusa US
Viongozi wa vyama vya siasa na wanaharakati nchini Pakistan wameonyesha kukerwa mno na matamshi ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu nchi yao.
Jumatatu ya jana Rais Donald Trump wa Marekani aliandika katika mtandao wa Twitter matamshi ya kuishambulia Pakistan kwamba, inawapatia hifadhi magaidi na kutishia kuikatia serikali ya nchi hiyo misaada ya kigeni. Shireen Mazari, mwakilishi na kiongozi wa ngazi ya juu wa chama cha 'Tahrik Insaf' kinachoongozwa na Imran Khan amesema kuhusiana na matamshi ya kuchukiza ya Trump kwamba, Pakistan imepoteza askari na raia wake wengi katika vita ambavyo haikutakiwa kuvishiriki pamoja na Marekani. Aidha Marazi ameitaka serikali ya Islamabad kuzuia huduma zote za mawasiliano ya anga na ardhi na Marekani.
Kwa upande wake Sherry Rehman, mmoja wa wajumbe wa chama cha Wananchi nchini Pakistan amejibu matamshi ya Trump kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba, Marekani inafanya njama ya kuihatarisha Pakistan. Naye Sheikh Rasheed Ahmad, mkuu wa chama cha 'Muslim League' nchini humo ameonyeshwa kukerwa na matamshi ya Trump na kusema kuwa, Washington haijajifunza namna ya kuamiliana na nchi nyingine. Hivi karibuni gazeti la New York Times liliandika kwamba, kuna uwezekano mkubwa Trump akakataa kutenga msaada wa Dola milioni 255 kwa ajili ya Pakistan.
Msuguano wa kisiasa kati ya Marekani na Pakistan uliibuka tangu alipoingia madarakani Rais Trump katika ikulu ya White House huku weledi wa mambo wakitahadharisha kwamba, tuhuma za Washington dhidi ya Islamabad zinajiri kupitia njama maalumu ambayo bado Wapakistan hawajaitambua.