Mpambe wa Trump mwenye chuki dhidi ya Waislamu ajiuzulu
Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Marekani aliyeteuliwa na Rais Donald Trump amelazimika kujiuzulu baada ya kanali ya televisheni ya CNN kufichua kanda ya sauti, ambapo anasikika akitoa maneno ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Carl Higbie amejiuzulu wadhifa aliotwikwa na Trump hivi karibuni wa Mkuu wa Masuala ya Nje wa Shirika la Kitaifa la Huduma za Jamii CNCS.
Msemaji wa CNCS, Samantha Jo Warfield, amethibitisha habari za kujiuzulu mpambe huyo wa Trump, ambaye alikuwa anasimamia taasisi kubwa zaidi ya masuala ya kijamii nchini Marekani. Baadhi ya taasisi za kujamii ambazo ziko chini ya shirika hilo ni pamoja na AmeriCops, Senior Corps na Mfuko wa Ubunifu wa Kijamii.
Carl Higbie alitangaza wazi wazi chuki zake dhidi ya Uislamu na Waislamu wakati alipokuwa akiendesha kipindi cha radio alichokiita "Sauti ya Uhuru" kati ya mwaka 2013 na 2014.
Baadhi ya matamshi hayo ya chuki aliyoyatoa wakati huo ni "Mimi siwapendi tu Waislamu", "Mimi ni kama Yesu, siwapendi Waislamu kwa kuwa idiolojia zao zinakera." Katika sehemu nyingine ya kanda hiyo ya sauti, mpambe huyo wa Trump anasikika akiutambulisha Uislamu kama dini inayounga mkono kulawitiwa watoto wadogo."
Kadhalika katika sehemu nyingine afisa huyo wa Marekani anasikika akifoka na kusema kwa hamaki kuwa: "Nyie Waislamu rudini katika shimo lenyu la choo mkaendelee kuwalawiti watoto wadogo kila Alkhamisi usiku!"
Si vibaya kuashiria hapa kuwa, Trump anaendelea kulaaniwa katika pembe mbali mbali za dunia, baada ya hivi karibuni kuzifananisha nchi za Afrika, Haiti na el-Salvador na shimo la choo.