Jaribio la kombora jipya la Marekani lafeli
https://parstoday.ir/sw/news/world-i39759-jaribio_la_kombora_jipya_la_marekani_lafeli
Jaribio la kombora jipya la Marekani lilifanywa jana katika jimbo la Hawaii la nchi hiyo limefeli.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 01, 2018 04:19 UTC
  • Jaribio la kombora jipya la Marekani lafeli

Jaribio la kombora jipya la Marekani lilifanywa jana katika jimbo la Hawaii la nchi hiyo limefeli.

Televisheni ya CNN ya Marekani imetangaza habari hiyo na kufafanua kuwa, mfumo wa Marekani wa kujilinda na mashambulizi ya makombora unaojulikana kwa jina la SM-3 ulifanyiwa majaribio jana kwa kufyatua kombora katika jimbo la Hawaii, hata hivyo kombora hilo limeshindwa kupiga shabaha iliyokusudiwa.

Duru za CNN zimesema kuwa, Wizara ya Ulinzi vya Marekani ilificha kufeli huko kutokana na hali ya wasiwasi iliyopo hivi sasa baina ya nchi hiyo na Korea Kaskazini.

 

Huko nyuma makombora ya Marekani yalikuwa yakifyatuliwa kutoka katika manuwari za kivita, lakini mara hii kombora hilo limefyatuliwa kutoka nchi kavu na kufeli. Ikumbukwe kuwa Japan ndiyo iliyokuwa inatarajiwa kununua mfumo huo wa Marekani wa kujilinda na mashambulizi ya makombora.

Mzozo baina ya Marekani na Korea Kaskazini umechachamaa zaidi katika miezi ya hivi karibuni kiasi kwamba majeshi ya nchi hizo mbili yamewekwa katika hali ya tahadhari hususan sehemu ambazo kuna hatari ya kushambuliwa kwa makombora.

Mara kwa mara Pyongyang imekuwa ikitishia kuishambulia Marekani kwa silaha za nyuklia hasa kila pale rais wa nchi hiyo Donald Trump anapopayuka na kutoa maneno ya kichochezi dhidi ya Korea Kaskazini.