Ripoti: Kila sekunde 98, mwanamke mmoja hubakwa na kudhalilishwa kijinsia Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i39837-ripoti_kila_sekunde_98_mwanamke_mmoja_hubakwa_na_kudhalilishwa_kijinsia_marekani
Ripoti iliyotolewa na Shirika la Habari la Huffington Post imeeleza kwamba katika kila sekunde 98, mwanamke mmoja nchini Marekani huwa anabakwa au kudhalilishwa kijinsia.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Feb 03, 2018 00:08 UTC
  • Ripoti: Kila sekunde 98, mwanamke mmoja hubakwa na kudhalilishwa kijinsia Marekani

Ripoti iliyotolewa na Shirika la Habari la Huffington Post imeeleza kwamba katika kila sekunde 98, mwanamke mmoja nchini Marekani huwa anabakwa au kudhalilishwa kijinsia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, tangu mwaka 1998 hadi sasa zaidi ya wanawake milioni 17.5 nchini Marekani wamekuwa wahanga wa vitendo vya ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia suala ambalo linatia wasi wasi mkubwa. Imezidi kufafanua kwamba asilimia 99 ya watu wanaofanya udhalilishaji huo wa kijinsia nchini humo, huwa hawachukuliwi hatua stahiki na badala yake huwa wanaachiliwa huru.

Wasichana wadogo, wahanga wakuu wa ubakaji Marekani

 

Kadhalika ripoti hiyo imesema kuwa asilimia 13 ya wanawake wote waliokumbwa na vitendo hivyo nchini Marekani hulazimika kujinyonga kutokana na kushindwa kuvumilia kuishi katika madhila hayo. Hii ni katika hali ambayo, wasichana wenye umri kati ya 16-19 nchini humo ndio ambao wanakabiliwa zaidi na hatari ya kubakwa na kudhalilishwa kijinsia tena mara nne zaidi ikilinganishwa na wanawake wengine. Marekani inaongoza katika jinai hizo dhidi ya wanawake kiasi kwamba, asilimia 20 ya wanawake wote wa nchi hiyo wamewahi kubakwa japo mara moja katika maisha yao.

Ripoti kama hiyo pia iliwahi kuandikwa na gazeti la The Guardian la nchini Uingereza miaka miwili iliyopita ambapo liliarifu kwamba kwa mujibu wa chunguzi, kila siku wanawake watatu nchini Marekani huuliwa na wanaume wenye mahusiano nao ya kijinsia au waliowafanyia vitendo vya udhalilishaji huo. Hayo yanajiri katika hali ambayo hadi sasa Marekani imekuwa ikijinadi kuwa eti ni msimamizi wa haki za binaadamu duniani, suala ambalo linakinzana wazi na uhalisia wa mambo.

Asilimia kubwa ya wabakaji nchini Marekani hawachukuliwi hatua za kweli za kisheria