Wademocrat waliotuhumiwa na Trump kuwa ni wahaini wachukizwa na matamshi hayo
Viongozi wa chama cha Democrat nchini Marekani, wamekosoa matamshi ya Rais Donald Trump aliyewataja kuwa ni wahaini na kusema kuwa, rais huyo anafuata mienendo ya udikteta.
Awali Trump aliwataja wawakilishi wa chama cha Democrat ambao hawakumpigia makofi wakati akitoa hotuba ya mwaka kuwa ni wahaini kwa taifa. Trump aliyasema hayo mjini Cincinnati, jimbo la Ohio na kusema: "Wao wanapendelea waone utendajikazi wa Trump ni mbaya katika nchi yetu inayoendelea. Wakati nikizungumzia maendeleo hayo ya nchi yetu wao walikuwa wakitoa radiamali hasi."
Kadhalika Trump aliongeza kwa kusema: "Ninaweza kuwataja watu wa namna hiyo kuwa ni wahaini. Kwa nini isiwe hivyo? Makusudio yangu ni kwamba, watu hao hawaipendi nchi yetu. Njooni tuzungumzie uhaini, inawezekana?" Alihoji Trump. Mgogoro kati ya Rais Donald Trump na viongozi wa chama cha Democrat umezidi kushtadi katika siku za hivi karibuni. Kufuatia hali hiyo, viongozi hao wa Democrat kwa upande wao wameyataja matamshi hayo kuwa ya udhalilishaji. Kadhalika viongozi hao wa Democrat wamemtaja rais huyo kuwa anayefuata mwenendo wa udikteta nchini Marekani.