EU, HRW na Amnesty zaitaka Bahrain imuachie huru mwanaharakati aliyeikosoa Saudia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i40751-eu_hrw_na_amnesty_zaitaka_bahrain_imuachie_huru_mwanaharakati_aliyeikosoa_saudia
Umoja wa Ulaya umeitaka serikali ya Bahrain imuachie huru Nabeel Rajab, mwanaharakati mashuhuri wa masuala ya haki za binadamu nchini humo, ambaye siku ya Jumatano alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kile kilichoelezwa kwamba, ni kupatikana na hatia ya uchochezi na kutoa jumbe za kukosoa utawala wa nchi hiyo na utawala wa Aal-Saud nchini Saudi Arabia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 23, 2018 04:05 UTC
  • EU, HRW na Amnesty zaitaka Bahrain imuachie huru mwanaharakati aliyeikosoa Saudia

Umoja wa Ulaya umeitaka serikali ya Bahrain imuachie huru Nabeel Rajab, mwanaharakati mashuhuri wa masuala ya haki za binadamu nchini humo, ambaye siku ya Jumatano alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kile kilichoelezwa kwamba, ni kupatikana na hatia ya uchochezi na kutoa jumbe za kukosoa utawala wa nchi hiyo na utawala wa Aal-Saud nchini Saudi Arabia.

Msemaji wa Kamisheni ya EU amesema kesi ya Rajab ni nembo ya kutoa hamasa kwa watetezi wa haki za binadamu wanaotaka kuheshimiwa uhuru wa kujieleza sio tu Bahrain, bali kote duniani. Amesema EU kwa mara nyingine tena inasisitizia udharura wa kuachiwa huru mwanaharakati huyo hususan kwa misingi ya ubinadamu, kutokana na kuzidi kuwa mbaya hali yake ya afya.

Wakati huo huo, Sarah Leah Whitson, Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch amesema hukumu mpya dhidi ya Nabeel Rajab ni kufungulia ukurasa mpya wa miaka kadhaa ya kuteswa, kunyanyaswa na kunyamazishwa watetea za haki za binadamu nchini Bahrain.

Naye Heba Morayef, Mkurugenzi wa Amnesty International eneo la Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika ameitaja hukumu hiyo dhidi ya Rajab kama ya fedheha na hujuma dhidi ya uhuru wa kujieleza, huku akisisitiza kuwa hukumu hiyo ni pigo kwenye uso wa haki.

Wabahrain wakiandamana kushinikiza kuachiwa huru Nabeel Rajab na wanaharakati wengine

Mahakama ya Bahrain imedai kwamba, Nabeel Rajab amepatikana na hatia ya makosa mengi kama vile kutoa maneno ya kuivunjia heshima nchi jirani (Saudia) na kueneza uzushi katika kipindi cha vita.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, katika kipindi cha miaka 6 iliyopita, zaidi ya raia elfu kumi na moja wa Baharain wamepokonywa uraia na kufukuzwa nchini humo kwa tuhuma zisizo na msingi wowote ule.