Wauzaji wa silaha za moto Marekani wapongeza msimamo hasi wa Trump
Chama cha Wauzaji Bunduki Marekani NRA kimepongeza pendekezo lililotolewa na Rais Donald Trump la kutaka kupewa silaha za moto walimu wa shule za nchi hiyo kwa ajili ya kuzuia msururu wa mashambulizi ya silaha za moto katika shule za nchi hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa chama hicho, Wayne LaPierre sanjari na kupongeza msimamo huo wa Trump, amewakosoa vikali wanasiasa wa chama cha Democratic wanaomshinikiza Trump aangalie upya suala la umiliki wa silaha za moto nchini humo.
LaPierre amesema wanasiasa hao wameingiza siasa kwenye suala muhimu la kumiliki bunduki, ambalo limeidhinishwa na kudhaminiwa kwenye katiba ya nchi hiyo.
Matamshi ya Trump ya kutaka walimu wapewa silaha za moto yamekosolewa na shakhsia mbalimbali nchini Marekani ambao wamemtaka badala yake aweke sheria kali za kudhibiti ununuzi na matumizi ya silaha za moto nchini Marekani.
Hivi karibuni kijana Nikolas Cruz mwenye umri wa miaka 19 alifanya shambulizi la kigaidi katika shule ya Stoneman Douglas jimboni Florida na kusababisha mauaji ya wanafunzi 17 na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa.
Takwimu zinasema kuwa, kwa mwaka maelfu ya watu huuawa au kujeruhiwa nchini Marekani kwa kupigwa risasi, nchi ambayo karibu silaha za moto milioni 270 hadi 300 ziko mikononi mwa raia.