Ufaransa yasisitiza kuheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA
Viongozi wa Ufaransa wamesisitiza tena misimamo yao juu ya kuyalinda na kuyaheshimu makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA).
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ufaransa imetoa taarifa ya kusisitiza msimamo wa nchi hiyo wa kuheshimu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA huku Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya nchi hiyo akitarajiwa kuwasili leo Jumatatu hapa Tehran kwa safari rasmi ya kkazi.
Taarifa hiyo imeeleza kwamba, Ufaransa inaheshimu na kufungamana na makubaliano hayo ya nyuklia yaliyofikiwa kati ya Iran na madola sita makubwa duniani na kwamba, inazitaka pande nyingine katika makubaliano hayo, nazo ziheshimu na kuhakikisha zinayatekeleza makubaliano hayo.
Sehemu nyingine ya taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Ufaransa imebainisha kwamba, Paris inalipa umuhimu suala la kuboreshwa uwekezaji na shughuli za kibiashara kati ya Ulaya na Iran.
Aidha taarifa hiyo imesema, Ufaransa ina matarajio kwamba, Iran itakuwa na nafasi chanya katika kupatiwa ufumbuzi migogoro ya Mashariki ya Kati.
Sehemu ya mwisho ya taarifa hiyo imeashiria safari ya leo hapa mjini Tehran ya Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Ufansa na kueleza kwamba, safari hii lengo lake ni kustawishwa zaidi uhusiano kati ya Tehran na Paris.
Taarifa hiyo imetolewa katika hali ambayo, hivi karibuni waziri huyo wa Mashauri ya Kigeni ya ufansa alitoa matamshi yaliyo dhidi ya Iran.