Mar 11, 2018 16:28 UTC
  • Wenye chuki dhidi ya Uislamu wachoma moto msikiti nchini Ujerumani

Katika kile kinachoonekana ni muendelezo wa matukio ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu barani Ulaya, wavamizi wasiojulikana wameuteketeza moto msikiti mmoja katika mji mkuu wa Ujerumani, Berlin.

Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, Msikiti wa Jamia wa Koca Sinan mjini Berlin umeshambuliwa na kuteketezwa kwa moto usiku wa kuamkia leo na 'watu wasioujulikana'.

Mashuhuda wanasema watu watatu waliokuwa wamefunika nyuso zao walivunja mlango wa msikiti huo na kurusha ndani kifaa kilichoripuka na kusababisha moto mkubwa kusambaa.

Polisi ya Ujerumani imesema inachunguza kiini cha tukio hilo, huku ikiwataka wakazi wa eneo hilo waisaidie kuwasaka wavamizi hao.

Wafuasi wa kundi la Pegida

Mashambulizi dhidi ya Waislamu na maeneo yao ya ibada na ya shughuli zao mbalimbali, yameongezeka sana katika siku za hivi karibuni sio tu Ujerumani, bali katika nchi nyingi za Magharibi.

Genge lenye chuki za kidini lijulikanalo kwa jina la PEGIDA limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Waislamu nchini Ujerumani.

Tags