Vitisho vipya vya Marekani dhidi ya Russia na China
Jenerali John E. Hyten Mkuu wa Kamandi ya Kistratijia ya Marekani (United States Strategic Command) sambamba na kubainisha kwamba China na Russia hazifahamu mahala zilipo nyambizi za nyuklia za Marekani, amesisitiza kuwa, nchi yake ina uwezo wa kuzisababishia hasara kubwa nchi hizo kwa kutumia makombora ya kutoka bara hadi bara yaliyomo kwenye nyambizi hizo.
Matamshi hayo ya Jenerali Hyten yametolewa ikiwa ni majibu kwa shaka iliyopo kuhusu uwezo wa Washington wa kutekeleza stratejia ya kijeshi ya 'Maangamizi Kamili ya Nyuklia ya Pande Mbili' kwa kimombo 'Mutually Assured Destruction (MAD)'. Kwa mujibu wa sera hiyo ambayo imekuwepo hadi sasa tangu enzi za Vita Baridi, utumiaji wa kila silaha za nyuklia zenye uwezo mkubwa unaofanywa na nchi mbili au kadhaa hasimu, utasababisha kuangamia kikamilifu mshambuliaji na mwenye kujihami. Matamshi ya kupenda vita ya afisa huyo wa jeshi la Marekani ni kielelezo kingine cha uhasama na uchokozi wa Marekani dhidi ya nchi nyingine hususan zile ambazo zinahesabiwa na Washington kuwa ni maadui zake katika ngazi ya kimataifa.
Aidha matamshi hayo ya Mkuu wa Kamandi ya Kistratijia ya Marekani si tu kwamba hayatasaidia kupunguza mizozo kati ya Marekani na Russia na China, bali yatazihamasisha Moscow na Beijing zijiimarishe zaidi kwa silaha za nyuklia ili kujilinda na kujihami na aina yoyote ya utumiaji wa Marekani wa silaha hizo hatari dhidi yao. Kuhusiana na suala hilo, Robert Soofer, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Marekani anasema: "Russia inatakiwa ifahamu kwamba shambulizi la silaha za nyuklia hata la mpaka maalumu, halitoiwezesha nchi hiyo kufikia malengo yake bali litapelekea kutokea mabadiliko ya msingi ya hali halisi ya uhasama na kuisababishia Moscow hasara isiyoweza kukadirika."
Baada ya matamshi ya hivi karibuni ya Rais Vladmir Putin wa Russia ambapo alijibu vitisho vya silaha za nyuklia vya Marekani dhidi ya nchi yake na kuweka bayana uwezekano wa Moscow kuanza kujizatiti kwa silaha hizo hatari, kundi la maseneta kadhaa wa Marekani sambamba na kuonyesha wasiwasi wao kuhusiana na suala hilo, walimtaka Rex W. Tillerson, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani kuanza mazungumzo na Russia juu ya uwezo wa kistratijia wa nchi hiyo. Hata hivyo Putin alifafanua kuwa, Russia itatumia silaha za nyuklia kujibu shambulizi la silaha kama hizo tu litakalofanywa dhidi yake na kwamba haitotumia silaha hizo za maangamizi kuanzisha hujuma za mashambulio. Katika nyaraka mpya kabisa ya sera za nyuklia za Marekani zinazoitwa ‘kuangaliwa upya hali ya silaha za nyuklia’, China, Russia, Korea Kaskazini na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimetajwa kuwa ni tishio kuu la kiusalama dhidi ya Marekani. Kadhalika nyaraka hiyo imebainisha kwamba mifumo mipya ya silaha za nyuklia za Russia za kutoka bara hadi bara ni moja ya tishio kubwa zaidi kwa Marekani.
Kuhusiana na suala hilo, Lisbeth Gronlund mtaalamu wa masuala ya nyuklia anaamini kwamba: “Trump anafuata njia ya kujifanyia mambo bila ya nadhari wala kujali chochote, njia ambayo, iwe ni hivi sasa au baada ya muda mrefu, itapunguza na kuhatarisha usalama wa Marekani.” Katika miaka ya karibuni uhusiano wa Russia na Marekani umekuwa ukishuhudia kushadidi mara kwa mara hitilafu na mivutano baina ya pande mbili; kiasi kwamba maslahi yanayokinzana ya madola hayo makubwa ya nyuklia yameifanya Marekani itumie stratijia zake mbalimbali ikiwa ni pamoja na ya usalama wa taifa, stratijia ya ulinzi wa taifa na sera mpya ya silaha za nyuklia kuitangaza Russia kuwa ni tishio kubwa kwa Marekani na pia tishio nambari moja la nyuklia dhidi ya nchi hiyo. Pamoja na hayo radiamali kali ya Rais Vladmir Putin wa Russia imewafanya viongozi wa Marekani wababaike na kuchukua misimamo ya kutapatapa. Matamshi ya Jenerali John E. Hyten Mkuu wa Kamandi ya Kistratijia ya Marekani (United States Strategic Command) yanaweza kutathminiwa katika uwanja huo.