Rais Duterte asema Ufilipino imejiondoa ICC
Rais Rodrigo Duterte wa Ufulipino amesema nchi yake imejiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, wiki chache baada ya chombo hicho kuanzisha uchunguzi wa 'jinai dhidi ya binadamu' dhidi ya washukiwa wa ulanguzi wa mihadarati, zinazodaiwa kufanywa na serikali.
Katika taarifa, Duterte amesema mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi haina mamlaka ya kuanzisha uchunguzi dhidi yake.
Amebainisha kuwa, ICC ni chombo kisichokuwa na maana kinachoendeshwa na Wamagharibi, huku akiukashifu Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kushughulikia masuala nyeti kama kuzima vita na machafuko katika sehemu mbalimbali duniani.
Rais wa Ufilipino amesema nchi za Magharibi zimekuwa zikiishutumu serikali yake kwa kupambana na mihadarati zikidai kuwa maafisa wa usalama wa nchi hiyo wanatumia mkono wa chuma kuwakabili washukiwa wa mihadarati.
Mwezi uliopita, ICC ilisema kuwa imeanzisha uchunguzi dhidi ya rais huyo wa Ufilipino, ikidai kuwa anabeba dhima ya mauaji ya watu elfu 20 wanaodaiwa kuuawa katika operesheni ya kupambana na walanguzi wa dawa za kulevya nchini humo.
Licha ya kuwa Ufilipino ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Roma uliobuni ICC, lakini Rais Rodrigo Duterte anasisitiza kuwa mkataba huo hauna itibari wala haujakuwa ukifuatwa nchini humo.
Kwa mujibu wa Mkataba wa Roma, mchakato wa nchi mwanachama kujiondoa ICC humalizika mwaka mmoja baada ya nchi husika kumtaarifu kwa barua rasmi Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.