Utafiti: Mamilioni kuhama Afrika na kuelekea Marekani na Ulaya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i42064-utafiti_mamilioni_kuhama_afrika_na_kuelekea_marekani_na_ulaya
Watafiti wanasema kuwa karibu watu milioni 1.5 wameondoka katika nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika na kuelekea Ulaya na Marekani tangu mwaka 2010, huku mamilioni ya wengine wakifanya mipango ya kufuata nyao za wenzao.
(last modified 2026-06-22T10:26:06+00:00 )
Mar 23, 2018 09:37 UTC
  • Utafiti: Mamilioni kuhama Afrika na kuelekea Marekani na Ulaya

Watafiti wanasema kuwa karibu watu milioni 1.5 wameondoka katika nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara barani Afrika na kuelekea Ulaya na Marekani tangu mwaka 2010, huku mamilioni ya wengine wakifanya mipango ya kufuata nyao za wenzao.

Nigeria, Ghana na Kenya ni nchi tatu ambako wahajiri wengi walitoka na kuelekea Ulaya na Marekani miongoni mwa makumi ya nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara.

Hayo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kituo cha utafiti cha PEW chenye makao yake mjini Washington. Utafiti huo umeonyesha kuwa, wimbi kubwa la watu katika nchi zilizo chini ya jangwa la Sahara kuelekea huko Magharibi limekuwa likiongezeka sana karibu kila mwaka tangu mwaka 2010. Wimbi hilo la wahajiri limeyumbisha rasilimali katika nchi zinazowapokea wahajiri hao ambazo zimekuwa zikihangaika kukidhi gharama za kuwahudumia raia hao.

Nchi za chini ya Jangwa la Sahara 

Aidha katika baadhi ya maeneo, wimbi la wahamiaji limechochea wasiwasi wa kisiasa na hivyo kumetolewa wito wa kufungwa mipaka ya nchi zinazopokea wahamiaji.

Wakimbizi hao wa Kiafrika wamekuwa wakiyahama makazi yao ya asili kutokana na kupoteza matumaini ya kupata ajira, kulipwa mishahara ya kiwango cha chini na kuwepo hatari ya kuibuka mizozo, migogoro ya kisiasa na utumwa mamboleo.

Phillip Connor mtafiti wa ngazi ya juu wa ripoti hiyo amesema kuwa mamilioni zaidi ya raia kutoka nchi za chini ya jangwa la Sahara wamesema kuwa, wangeondoka katika nchi zao na kuelekea Ulaya na Marekani kama wangeweza.