Watu 3 wauawa Ufaransa katika mashambulizi ya Daesh
Watu watatu wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya mtu aliyekuwa na silaha kushambulia duka moja kubwa na kuwafyatulia risasi polisi huko kusini magharibi mwa Ufaransa.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa imethibitisha kuwa, watu watatu wameuawa katika shambulizi hilo na kwamba kuna uwezekano hali ikawa mbaya zaidi kutokana na majeruhi watatu wa shambulizi hilo ambao hali ya baadhi yao imeripotiwa kuwa mbaya sana.
Muda mfupi baada ya shambulizi hilo polisi ya Ufarasna ilivamia duka hilo na Waziri wa Mambo ya Ndandi wa Ufaransa, Gerard Collomb amethibitisha kuwa maafisa usalama wamemuua mhusika wa shambulizi hilo.
Rais Emmanuel Macron pia amesema, tukio hilo linaonekana kuwa la kigaidi na kwamba vyombo husika vinalinda usalama katika eneo hilo.
Mtekelezaji wa shambulizi hilo ambaye amesema ni mwanachama wa kundi la kigaidi la Daesh, ametaka kuachiwa huru Salah Abdeslam, mshukiwa mkuu wa shambulizi la kigaidi la mwaka 2015 mjini Paris ambalo liliua watu wasiopungua 130.
Awali mshambuliaji huyo aliwapiga risasi maafisa wanne wa polisi katika mji wa kihistoria wa Carcassonne na baadaye akavamia dula kubwa la bidhaa katika mji wa Trebes.
Zaidi ya watu 240 wameuawa katika mashambulizi kadhaa ya kigaidi yanayofanywa na wanachama au wafuasi wa kundi la kigaidi la Daesh nchini Ufaransa tangu mwaka 2015.