Rais wa Ufilipino atishia kumkamata Mwendesha Mashtaka wa ICC
Rais wa Ufilipino amesema atamtia mbaroni Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC, iwapo atatia guu katika nchi hiyo kwa ajili ya kuchunguza tuhuma zinazomkabili rais huyo.
Katika kikao na waandishi wa habari jijini Manila jana Ijumaa, Rais Rodrigo Duterte amesisitiza kuwa, "Mwendesha Mashtaka huyo (Fatou Bensouda) wa mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague nchini Uholanzi hana mamlaka ya kuanzisha uchunguzi dhidi yangu."
Amemuonya kwa kusema, "Usije hapa kufanya uchunguzi wa madai ambayo hayana msingi. Hatua hiyo ni kinyume cha sheria. Usikanyage hapa kabisa, nitakukamata."
Rais wa Ufilipino amekariri kuwa, ICC ni chombo kisichokuwa na maana kinachoendeshwa na Wamagharibi, huku akiukashifu Umoja wa Mataifa kwa kushindwa kushughulikia masuala nyeti kama kuzima vita na machafuko katika sehemu mbalimbali duniani.
Mwezi uliopita, Duterte alisema nchi yake imejiondoa kwenye Mkataba wa Roma uliounda ICC, wiki chache baada ya chombo hicho kuanzisha uchunguzi wa 'jinai za kibinadamu dhidi ya washukiwa wa ulanguzi wa mihadarati', zinazodaiwa kufanywa na serikali.
ICC inasema kuwa imeanzisha uchunguzi dhidi ya rais huyo wa Ufilipino, ikidai kuwa anabeba dhima ya mauaji ya watu elfu 20 wanaodaiwa kuuawa katika operesheni ya kupambana na walanguzi wa dawa za kulevya nchini humo.