Azma ya kimataifa kwa ajili ya kulinda mapatano ya JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/world-i43670-azma_ya_kimataifa_kwa_ajili_ya_kulinda_mapatano_ya_jcpoa
Huku tarehe 12 Mei ikiwa inakaribia, ambayo ni tarehe ya mwisho iliyoainishwa na Rais Donald Trump wa Marekani kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi sita kubwa za dunia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA, radiamali na harakati za serikali na viongozi wa kundi la 5+1 kwa ajili ya kulinda mapatano hayo zimeongezeka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 26, 2018 08:41 UTC
  • Azma ya kimataifa kwa ajili ya kulinda mapatano ya JCPOA

Huku tarehe 12 Mei ikiwa inakaribia, ambayo ni tarehe ya mwisho iliyoainishwa na Rais Donald Trump wa Marekani kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na nchi sita kubwa za dunia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA, radiamali na harakati za serikali na viongozi wa kundi la 5+1 kwa ajili ya kulinda mapatano hayo zimeongezeka.

Viongozi wa Russia na wa Umoja wa Ulaya ni miongoni mwa shakhsia muhimu wa kimataifa ambao wanataka kulindwa mazungumzo hayo muhimu ya kimataifa. Akizungumzia suala hilo hapo siku ya Jumatano, Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuimarishwa mapatano ya JCPOA, kulindwa na kudhaminiwa masharti yake yote katika mfumo wa hivi sasa ni jambo la dharura kwa serikali ya Moscow. Katika upande wa pili, Vladimir Chizhov, mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Ulaya amesema hakuna  nchi yoyote iliyo na haki ya kutangaza msimamo wa upande mmoja kwa niaba ya kundi la 5+1 na kusisitiza kuwa si Marekani wala nchi za Ulaya zina ruhusa ya kubadilisha vipengee vya mapatano ya JCPOA. Akizungumza Jumatano, Federica Mogherini, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya alisema siku ya Jumatano ikiwa ni katika radiamali yake dhidi ya matamshi yaliyotolewa katika mazungumzo ya Marais Donald Trump wa Marekani na Emmanuel Macron wa Ufaransa kuhusiana na mpango wa kutayarishwa mapatano mengine ya nyuklia na Iran, na kusisitiza kwamba, kwa sasa kuna mapapatano mamoja tu ya JCPOA na ambayo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa na kwamba yanapaswa kuheshimiwa na kulindwa.

Marais Macron na Trump katika mazungumzo yao ya hivi karibuni

Macron pia amesisitiza kwamba Ufaransa haitajiondoa kwenye mapatano hayo kwa njia yoyote ile. Makubaliano ya Iran na kundi la 5+1 yalianza kutekelezwa Januari 2016 lakini Marekani ambayo ni moja ya nchi wanachama wa kundi hilo haijatekeleza ahadi ilizotoa kuhusiana na makubaliano hayo na sasa Trump anatishia kujitoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa. Tishio hilo mbali na kukabiliwa na radiamali kali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia limekosolewa na jamii ya kimataifa. Trump amekuwa akitoa masharti ya ziada na yaliyo kinyume cha sheria ambayo hayajaainishwa katika makubaliano ya JCPOA na kutoa muhula wa hadi kufikia Mei 12 yawe yametekelezwa na wakati huo huo kufanya juhudi zake zote kwa ajili ya kuwashawishi washirika wake wa Ulaya waishinikize Iran ikubali matakwa haramu ya Washington.

Nchi za kundi la 5+1

Kwa maneno ya Richard Sokolsky, mtaalamu wa masual ya kisiasa, Trump anasisitiza juu ya kujitoa kwenye mapatano ya JCPOA na kukabiliana na Iran Mashariki ya Kati katika hali ambayo yeye mwenyewe hana malengo wala stratijia maalum kuhusiana na suala hilo. Hata nchi za Ulaya ambazo zimekiri kwamba Iran imetekeleza ahadi zake zote kuhusiana na makubaliano ya JCPOA hazikubaliani na siasa hizo za Trump. Hata hivyo nchi tatu za Ulaya za kundi la 5+1 yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimekubaliana na Marekani kwa ajili ya kutoa mashinikizo dhidi ya Iran kuhusiana na mpango wake wa makombora na sera zake za kieno, kwa ajili ya kumridhisha Trump na wakati huohuo kulinda makubaliano ya JCPOA. Pamoja na hayo nchi hizo zinaashiria kwamba kuna uwezekano mdogo wa Trump kuendelea kubakia katika makubaliano hayo.

Mtambo wa nishati ya nyuklia wa Bushehr nchini Iran

Matamshi na misimamo ya viongozi wa serikali na taasisi za kimataifa inabainisha wazi kwamba jamii ya kimataifa inapinga mitazamo isiyo ya kimantiki na ya kujitakia makuu Trump kuhusiana na ima mapatano ya JCPOA yafanyiwe marekebisho au Marekani ijitoe katika mapatano hayo. Kwa msingi huo Marekani kwa mara nyingine tena imekwenda kinyume na matakwa ya jamii ya kimataifa kwa kutaka kulazimisha mitazamo yake ya upande mmoja kwa wanachama wengine wa kundi la 5+1. Hata washirika wa Ulaya wa Marekani wanakiri kwamba msimamo huo wa Trump unakwenda kinyume na ahadi zilizotolewa na Marekani katika kipindi cha uongozi wa Barack Obama katika fremu ya azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na vilevile sheria za kimataifa, yaani zinazosisitiza udharura wa kutekelezwa ahadi zinazotolewa na serikali.