Kansela wa Ujerumani Merkel apoteza matumaini kuhusu Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i44336-kansela_wa_ujerumani_merkel_apoteza_matumaini_kuhusu_marekani
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kwa mara nyingine amesema nchi za Ulaya haziwezi kuendelea kuitegemea Marekani katika masuala ya kijeshi na kujihami. Merkel amewataka waitifaki wa Ujerumani barani Ulaya wachukue hatima ya bara hilo mikononi mwao kwani Marekani haiwezi kutegemewa tena.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 11, 2018 03:44 UTC
  • Kansela wa Ujerumani Merkel apoteza matumaini kuhusu Marekani

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani kwa mara nyingine amesema nchi za Ulaya haziwezi kuendelea kuitegemea Marekani katika masuala ya kijeshi na kujihami. Merkel amewataka waitifaki wa Ujerumani barani Ulaya wachukue hatima ya bara hilo mikononi mwao kwani Marekani haiwezi kutegemewa tena.

Hali kadhalika Merkel amebainisha wasiwasi wake kuwa, mwenendo wa hivi sasa wa Marekani katika zama za utawala wa Donald Trump unaonyesha kuwepo ufa mkubwa unaozidi kupanuka baina ya Ulaya na Marekani kuhusu masuala mbali mbali. Muelekeo wa Trump kuhusu masuala mengi unakinzana na sera za rais aliyemtangulia, Barack Obama.

Hitilafu baina ya Marekani ya Trump na Umoja wa Ulaya zinadhihirika wazi zaidi katika uhusiano  na nchi mbili muhimu za bara hilo yaani Ujerumani na Ufaransa.

Kumekuwepo na mgongano mkubwa baina ya utawala wa Trump na Umoja wa Ulaya kuhusu masuala muhimu ya uhusiano wa pande mbili na pia masuala kadhaa ya kimataifa. Hali hiyo imepelekea kuibuka mabadiliko katika uhusiano wa kistratijia baina ya Ulaya na Marekani.  Kati ya hitilafu hizo ni pamoja na nafasi ya Ulaya katika muungano wa kijeshi wa NATO unaoongozwa na Marekani, uhusiano na Russia, mapatano ya tabia nchi ya Paris na pia kuhusu mapatano ya nyuklia ya Iran maarufu kama JCPOA.

Katika nukta hizo zote Trump amekuwa akifuatilia tu misimamo yake binafsi huku akipuuza wazi wazi misimamo  ya nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zimekuwa waitifaki wa muda mrefu katika muungano wa NATO.

Kwa mtazamo wa Hassan Abedini mtaalamu wa masuala ya kimataifa, hitilafu baina ya Umoja wa Ulaya na Marekani katika kipindi cha utawala wa Trump haziko tu katika masuala ya kibiashasra bali pia katika masuala ya kisiasa, kidiplomasia, kiusalama na hata kijamii."

Hitilafu hizo zimewakasirisha sana wakuu wa Ulaya hasa Kansela Angela Merkel wa Ujerumani. Mitazamo ya Merkel inahitiliafiana kikamilifu na ile ya Trump kuhusu uhusiano baina ya nchi mbili, masuala ya Ulaya na masuala ya kimataifa.

Trump anaamini kuwa sera za upande mmoja na za ubinfasi zitapelekea nguvu za Marekani kuimarika duniani. Ni kwa msingi huo ndio Merkel akaonekana kupoteza matumaini na kupelekea atoe matamshi Alhamisi akisisitiza tena ulazima wa Umoja wa Ulaya kuwa na sera za kujitegemea.

Hivi sasa imebainika wazi kuwa muelekeo wa mustakabali wa Ulaya na Marekani katika utawala wa Trump utakuwa ni kutengana pande hizo mbili katika masuala muhimu. Kwa msingi huo nchi za Ulaya zinapaswa kuimarisha umoja na mshikamano ili kukabiliana na sera za Trump katika uga wa kimataifa. Hilo linatazamiwa kujitokeza wazi katika kadhia ya mpatano ya nyuklia ya Iran ambapo Trump amesisitiza kutekeleza sera zake dhidi ya mapatano hayo jambo ambalo limethibitisha wazi sera zake za maamuzi ya upande mmoja na kupuuza maslahi ya nchi zingine hata zile ambazo zimekuwa waitifaki wa Washington kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Stephen Blank mtaalamu katika Baraza la Uhusiano wa Kigeni la Marekani, hatua ya Trump kuyahujumu mapatano ya nyuklia ya Iran itapelekea kuibuka mvutano baina ya Washington na Ulaya, Russia pamoja na China.

Nchi za Ulaya sasa zinafahamu fika kuwa, maamuzi ya Trump yanachukuliwa tu kwa kuzingatia maslahi ya Marekani pasina kuzingatia maslahi ya Ulaya. Katika siku za usoni tunatazamia kushuhudia msuguano mkali baina ya Marekani na Ulaya kuhusu masuala ya biashara. Kwa hivyo  msimamo uliochukuliwa na Merkel ni ishara kuwa nchi za Ulaya zitajitenga na Marekani kuhusu masuala mengi muhimu.