Majibu makali ya Russia kwa vikwazo vipya vya Marekani
Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetoa tamko kali la kujibu vikwazo vipya vya Marekani dhidi yake na kusema kuwa, vikwazo hivyo vya serikali ya Donald Trump dhidi ya Moscow vinatokana na hamaki za Washington za kushindwa mashambulizi yake ya tarehe 14 Aprili nchini Syria.
Itakumbukwa kuwa siku ya Jumatano ya tarehe 9 mwezi huu wa Mei, Marekani ilizidi kuonesha chuki zake dhidi ya Russia kwa kuviwekea vikwazo baadhi ya vituo na duru za kijeshi za Russia na baadhi ya mashirika ya nchi hiyo kwa kile kilichodaiwa na Washington kuwa ni "kuvunja sheria za Marekani za kuzuia uenezaji wa silaha za mauaji ya umati."
Inavyoonekana ni kwamba Marekani iko tayari kutumia kisingizio chochote kile kuhalalisha kuiwekea vikwazo zaidi Russia. Kisingizio kilichotumiwa sasa hivi na Marekani ni hatua ya Russia ya kuweka mikataba na baadhi ya nchi duniani ambayo inakinzana na sheria za ndani ya Marekani. Alaakullihaal, Moscow inaona kuwa, vikwazo hivyo vipya vya Marekani dhidi yake vinatokana na hamaki za Marekani baada ya Russia kuimarisha mfumo wa kijeshi wa Syria wa kujilinda na mashambulizi ya makombora na jinsi mfumo huo ulivyofanikiwa sana kukabiliana na mashambulio ya tarehe 14 Machi yaliyofanywa na Marekani, Uingereza na Ufaransa dhidi ya Syria. Moscow inasema, vikwazo vya namna hiyo kamwe haviwezi kuilazimisha ibadilishe msimamo wake wa kuwaimarisha marafiki zake, kwani kuwaimarisha waitifaki wake kijeshi kuna uhusiano wa moja kwa moja na manufaa ya kitaifa ya Russia. Mara kwa mara Moscow imekuwa ikilaani ujuba na jeuri ya rais wa Marekani, Donald Trump ya kutumia mabavu na vikwazo kuzishinikiza nchi nyingine. Vile vile Russia inaamini kuwa, mbinu hizo zinazotumiwa na Marekani kamwe haziwezi kuilazimisha Moscow kubadilisha siasa na misimamo yake. Hivi sasa uhusiano wa Marekani na Russia unaonekana unazidi kuwa mbaya siku baada ya siku kiasi kwamba sasa hivi umezidi kuharibika katika nyuga tofauti za kisiasa, kidiplomasia, kibiashara, kiuchumi, kijeshi na kiusalama.
Sergey Rogov, mhadhiri wa vyuo vikuu katika somo la Sayansi ya Siasa anaamini kuwa, hivi sasa vita vipya baridi vinaendelea baina ya Marekani na Russia.
Vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Russia vinaonesha kuwa Washington imeazimia kuiwekea vikwazo Moscow hata kwa sababu ambazo haziingiliki akilini kama hivyo kuitaka Russia iheshimu na ifuate sheria za ndani ya Marekani. Hilo linaonekana wazi tangu mwaka 2014 ambapo Marekani imekuwa ikiiwekea vikwazo Russia kwa kutumia visingizio kama kukubaliana Moscow na uamuzi wa wananchi wa eneo la Crimea wa kujiunga na ardhi ya Russia, au kujihusisha Moscow na mgogoro wa Ukraine, na muhimu kuliko yote, hatua ya Russia ya kueneza ushawishi wake kupitia nchi waitifaki wake kama vile Syria.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergei Ryabkov anaamini kuwa, Donald Trump anatenda kinyume kabisa na ahadi alizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi, na siasa za mambo ya nje za Marekani hivi sasa ni mbaya zaidi kuliko za kipindi cha Barack Obama.
Wakati huo huo, Alexey Mukhin, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa nchini Russia anaamini kuwa, watu wanaopanga vikwazo vipya dhidi ya Moscow huko Marekani, wanafanya kosa kubwa.
Kiujumla ni kwamba, uwepo wa kijeshi wa Russia wenye taathira kubwa huko Syria na misaada yake kwa jeshi la nchi hiyo iliyoitia nguvu Damascus na kuiwezesha kukabiliana vizuri na mashambulizi ya anga na ya makombora ya nchi za Magharibi na utawala wa Kizayuni wa Israel ni mambo ambayo yameihamakisha sana Marekani na hivi sasa inatumia vikwazo kuvuruga jambo hilo. Hata hivyo, vikwazo hivyo vipya si tu vinaonekana haviwezi kuiteteresha Russia, lakini vimeifanya Moscow nayo ichukue hatua za kujibu vikwazo hivyo na kuvigeuza vitisho vya Marekani kuwa fursa nzuri kwake ya kujiimarisha zaidi. Moscow imeonesha wazi kuwa haina nia kabisa ya kulegeza kamba katika malengo yake makuu ikiwemo msimamo wake wa kulinda maslahi yake ya kitaifa nchini Syria hata kama jambo hilo litaendelea kuihamakisha Marekani.